1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miripuko ya kemikali yauwa 44 China

13 Agosti 2015

Watu 44 wameuawa na wengine zaidi ya 500 wamejeruhiwa katika miripuko mikubwa uliotokea jana jioni katika eneo la viwanda mjini Tianjin Kaskazini mwa China. Mali yenye thamani kubwa pia imeteketezwa katika mripuko huo.

https://p.dw.com/p/1GErU
Miripuko miwili iliyotokea imesababisha moto mkubwa
Miripuko miwili iliyotokea imesababisha moto mkubwaPicha: Reuters

Miripuko miwili mikubwa imetokea katika eneo lenye maghala ya kemikali za sumu pamoja na matangi ya gesi katika mji huo wa Tianjin, ambao una bandari ya 10 kwa ukubwa duniani. Wazima moto 12 ni miongoni mwa watu 44 ambao imethibitishwa kuwa wameuawa na miripuko hiyo.

Taarifa ya utawala wa jimbo la Tianjin imesema watu 520 wamejeruhiwa katika ajali hiyo ya miripuko, huku 60 kati yao wakiwa katika hali mahtuti. Gazeti la kila siku la People's Daily, limeripoti kuwa bado moto ulikuwa ukiendelea kuwaka sehemu nne tofauti. Mmoja wa wafanyakazi katika eneo lililoathirika, Wu Dejun ameeleza jinsi alivyonusurika.

''Nimeona moto kwa mbali, na ghafla ukatokea mripuko. Wazo la kwanza kichwani mwangu lilikuwa kukimbia. Mara nikasikia mripuko wa pili. Nilikurupuka kama mwendawazimu. Damu ilikuwa imejaa mwilini mwangu. Rafiki zangu walinipeleka hospitali'', amesema Wu.

Serikali yaingilia kati

Rais wa China Xi Jinping ametoa agizo kwa mamlaka zinazohusika kutumia uwezo wao wote kuwaokoa watu waliojeruhiwa na kuwatibu, na kuhakikisha usalama wa watu na mali yao.

Uharibifu uliosababishwa na ajali hiyo ya miripuko katika eneo jirani
Uharibifu uliosababishwa na ajali hiyo ya miripuko katika eneo jiraniPicha: Reuters/J. Lee

Shirika la habari la serikali ya China la Beijing News limenukuu idara ya wazima moto mjini Tianjin, iliyosema kuwa imepoteza mawasiliano na wazimamoto 36, na kwamba wengine 33 ni miongoni mwa majeruhi wanaotibiwa hospitalini.

Nalo Xinhua, Shirika rasmi la habari la China, limeripoti kwamba wazimamoto 1,000 wanaotumia magari 140, walikuwa wakiendelea kupambana kuuzima moto. Kituo cha televisheni cha China, CCTV kimeripoti kuwa afisa mmoja wa kampuni husika amekamatwa.

Ukubwa mithili ya tetemeko

Miripuko hiyo ilikuwa mikubwa kiasi cha kunaswa na satelaiti zilizo angani, na imesababasha mtikisiko katika nyumba zilizo umbali wa kilomita kadhaa katika mji wa bandari wa Tianjin, wenye wakazi milioni 15. Kituo cha Marekani cha uchunguzi wa kijiolojia umeitafsiri miripuko hiyo kama tetemeko la ardhi.

Wakazi wa maeneo yaliyoathirika wamkiwa wamefadhaishwa na athari za miripuko
Wakazi wa maeneo yaliyoathirika wamkiwa wamefadhaishwa na athari za miripukoPicha: Reuters

Licha ya ajali hiyo, bandari ya Tinjian imeendelea kufanya kazi kama kawaida, hii ikiwa ni kwa mujibu wa maafisa wa bandari hiyo, ambayo ni lango muhimu kwa eneo la Kaskazini mwa China.

Idara ya zima moto ya China imesema moto umezuka usiku saa tano kasoro dakika 10 saa ya eneo hilo, katika maghala ya kuhifadhi aina ya kemikali zenye hatari, na kwamba miripuko ilifuata baadaye.

Ofisi ya China inayochunguza tetemeko la ardhi imesema mripuko wa kwanza ulikuwa mithili ya mpasuko wa tani 3 za baruti kali, huku wa pili ukilinganishwa na mripuko wa tani 21 za baruti hiyo.

Ajali za kiviwanda sio jambo lisilo la kawaida nchini China, ambako kumeshuhudiwa miongo mitatu ya ukuaji wa haraka wa uchumi. Mripuko mwingine uliotokea mwaka jana katika kiwanda cha vipuri vya magari uliwauwa watu 75.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/dpae

Mhariri:Josephat Charo