1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yataka machafuko yasitishwe nchini Syria

18 Februari 2012

China imesema leo Jumamosi (18.02.2012) kuwa inaunga mkono mipango ya Rais wa Syria Bashar al-Assad, kuandaa kura ya maoni kuhusu katiba mpya na uchaguzi utakaokubalia mfumo wa vyama vingi vya kisiasa

https://p.dw.com/p/145Mz
Eneo la mripuko wa bomu nchini Syria
Eneo la mripuko wa bomu nchini SyriaPicha: Reuters

Waziri Msaidizi wa Mambo ya Nchi za Nje wa China, Zhai Jun, ambaye alifanya mazungumzo na Rais wa Syria, Bashar al-Assad, mjini Damascus leo Jumamosi pia ametoa wito kwa pande zote nchini Syria kusitisha machafuko.

Hayo yamejiri siku moja tu baada ya machafuko ambayo kundi moja la kutetea haki za binadamu,kusema yamewauwa takribani watu 30. Maandamano pia yamesambaa hadi maeneo jirani ya mji mkuu Damascus kwa mara ya kwanza, na vikosi vya usalama vimeushambulia tena mji wa Homs. Jun amesema baada ya mazungumzo na Assad kuwa msimamo wa China ni kuitaka serikali ya Syria, upinzani, na waasi kusitisha vitendo vyao vya machafuko mara moja.

China: utulivu urejeshwe haraka

Televisheni ya taifa ilimnukuu Zhai akisema kwamba ni muhimu utulivu urejeshwe haraka iwezekanavyo kwa sababu hilo litatimiza matakwa ya Wasyria.

Naibu waziri wa mambo ya nje wa China Zhai Jun akiwa nchini Syria
Naibu waziri wa mambo ya nje wa China Zhai Jun akiwa nchini SyriaPicha: dapd

Aliongeza kuwa wanatarajia kuona kura ya maoni kuhusu katiba mpya pamoja na uchaguzi wa ubunge ukifanyika kwa njia ya amani. China ilijiunga na Urusi mara mbili kuzuia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kulaani ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Assad katika maasi yaliyodumu miezi 11.

Jana Alhamisi, makundi ya upinzani nchini Syria yalikataa rasimu mpya ya katiba ambayo inaweza kumaliza takriban miongo mitano ya utawala wa chama kimoja cha kisiasa, na yakawataka wapiga kura kususia zoezi la kura ya maoni ya Februari 26. Wanaharakati wameiitisha siku ya uasi kesho Jumapili mjini Damascus ili kuunga mkono harakati za maandamano.

Wanajeshi wa serikali wawafyatulia risasi waandamanaji

Wakati huo huo, vikosi vya Syria vimefyatua risasi za moto kuwatawanya waandamanaji dhidi ya rais Bashar al-Assad katika mji mkuu Damascus, ambapo watu wanne wamejeruhiwa. Ufyatuaji huo wa risasi ulitokea katika mazishi ya vijana watatu waliouwawa kwenye maandamano ya hapo jana Ijumaa dhidi ya Assad. Takriban waandamanaji 30,000 waliingia barabarani mjini Mezze kuomboleza vifo vya vijana hao waliouwawa katika mji mkuu wa Damascus.

Vikosi vya serikali ya Syria
Vikosi vya serikali ya SyriaPicha: dapd

Na wakati hayo yakishuhudiwa, Marekani imezipeleka nchini Syria ndege zisizoendeshwa na marubani ili kutathmini ukandamizaji unaoendelea kufanywa na wanajeshi wa serikali dhidi ya raia. Maafisa wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani wameiambia televisheni ya Marekani (NBC) kuwa ndege hizo zinakusanya ushahidi ambao unaweza kutumiwa kutayarisha kesi inayoweza kshughulikiwa na jamii ya kimataifa. 

Mwandishi: Bruce Amani/dpa/Reuters

Mhariri: Ndovie, Pendo Paul