1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China ni gereza kubwa la waandishi wa habari

Admin.WagnerD16 Desemba 2015

China,Misri na Iran ndizo nchi zinaongoza kwa kuwafunga gerezani waandishi wa habari kulingana na ripoti ya shirika la kutetea haki za waandishi wa habari jijini New York, Committee to Protect Journalists.

https://p.dw.com/p/1HNmE
China Prozess Pu Zhiqiang
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Wong

Ripoti hiyo ambayo imetolewa leo, pia inaorodhesha Eritria,Ethiopia na Uturuki kwenye orodha hiyo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 25 ya waandishi wa habari 199 ulimwenguni waliokuwa gerezani kufikia Disemba mosi kuhusiana nakazi yao wako nchini China.Nchi hiyo inayotawaliwa na chama cha kikoministi chini ya uongozi wa Rais Xi Jinping ilikuwa na waandishi wa habari 49 gerezani ,idadi ambayo ni kubwa kwa China tangu shirika hilo lianze kutoa ripoti zake kila mwaka tangu 1990.

Hata hivyo Kulingana na ripoti hiyo,idadi hiyo imepungua na ni waandishi habari wachache wamefungwa gerezani mwaka huu ingawa idadi ya walioshikwa mateka imeongezeka,huku ikitaja China kuwa gereza kubwa zaidi la waandishi wa habari ulimwenguni ikifuatiwa na Misri.

Aidha, imewataja wachina watatu walioko gerezani ambao hawakujumuishwa kwenye orodha hiyo ya kila mwaka ambao ni ndugu watatu wa mwandishi wa Marekani anayefanya kazi na shirika la Radio Free Asia anayeangazia jinsi China inavyowatendea watu wa jamii yake ya Uighurs ambao ni waislamu .CPJ imetaja kufungwa kwa ndugu za Shohret Hoshur kama kitendo cha kulipiza kisasi kufuatia namna anavyoripoti na kwamba huu ni mfano wa yale China inaweza kuyafanya ili kunyamazisha wakosoaji wake.

Misri ina mazingira mabaya kwa waandishi habari

Misri ni ya pili kwenye orodha hiyo huku ikiwa imewaweka waandishi 23 gerezani, hii ikiwa ni idadi ya juu ukilinganisha na miaka kumi iliyopita ambapo hata mwaka 2012 hakukuwa na kisa chochote cha kuwaweka gerezani waandishi wa habari.Ripoti hiyo inasema huenda hakuna mahala palipo na mazingira mabaya zaidi kwa waandishi wa habari kama ilivyo nchini Misri huku ikishutumu Rais Abdel Fattah el-Sissi kwa kuchukua hatua hizo kwa kisingizio cha usalama wa taifa tangu aliposhika hatamu mwaka 2014, mwaka mmoja baada ya jeshi la nchi hiyo kumuoandoa mamlakani Rais Mohammed Morsi anayetoka katika kundi la Udugu wa Kiislamu.

Mwezi Agosti ,el-Sissi aliidhinisha sheria ambayo miongoni mwa mambo mengine inaruhusu kuwatoza faini za juu waandishi wa habari ambao hawatafuata mkondo wa serikali.

Mwandishi wa habari wa gazeti la Washington Post Jason Rezaian ni mmoja wa waandishi wa habari 19 ambao shirika la CPJ limewaorodhesha kuwekwa gerezani nchini Iran, chini ya kiongozi wa kidini Ayatolla Ali Khamenei na Rais Hassan Rouhani.

Ripoti hiyo vile vile imetaja Eritrea katika Afrika mashariki kuwa nchi inayokaidi zaidi sheria ulimwenguni kwani hakuna mwandishi wa habari aliyeorodheshwa na CPJ aliyewekwa gerezani chini ya utawala wa muda mrefu wa Rais Isaias Afwerki, ambaye amefikishwa mahakamani na kufunguliwa mashitaka. Shirika hilo linasema waandishi habari 17 wamko gerezani nchini humo.

Mwandishi:Bernard Maranga/AP/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba