1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chuki na ufurukutwa wa kidini waongezeka Marekani?

Admin.WagnerD10 Januari 2011

Mahusiano kati ya dini tafauti, kura ya maoni ya Sudan ya Kusini na jaribio la mauaji dhidi ya mjumbe wa Bunge la Marekani, Gabrielle Giffords, ni miongoni mwa mada katika magazeti ya leo, 10 Januari 2011, ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/zvmH
Gabrielle Giffords akiwapungia mkono wafuasi wake katika jiji la Washington D.C, katika picha hii ya mwaka 2010 Hivi sasa Giffords yuko mahututi hospitali, baada ya kupigwa risasi kichwani
Gabrielle Giffords akiwapungia mkono wafuasi wake katika jiji la Washington D.C, katika picha hii ya mwaka 2010 Hivi sasa Giffords yuko mahututi hospitali, baada ya kupigwa risasi kichwaniPicha: dapd

Gazeti la Westdeutsche Allgemeine, linasema kwamba, mashambulizi dhidi ya waumini wa Kikristo, katika nchi za Iraq na Misri mwishoni mwa mwaka 2010, yataendelea kutawala mijadala kwa siku kadhaa zijazo.

Linamnukulu kiongozi wa Baraza la Makanisa hapa Ujerumani, Margot Käßmann, akiwataka viongozi wa Ujerumani, kukutana kwa makusudi na makundi ya dini ya Kikristo, pale wanapotembelea nchi ambazo Wakristo ni wachache, ili kupata taarifa halisi, za namna waumini hao wanavyotendewa.

"Kila Muislam ana haki ya kutekeleza imani yake hapa Ujerumani, lakini pia tungependa kuona kuwa Wakristo nao wana haki hiyo hiyo, popote pale walipo duniani." Anasema Käßmann.

Wakaazi wa Sudan ya Kusini wakiwa katika foleni ya kusubiri kupiga kura ya maoni, Jumapili 9 januari 2011
Wakaazi wa Sudan ya Kusini wakiwa katika foleni ya kusubiri kupiga kura ya maoni, Jumapili 9 januari 2011Picha: AP

Mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker anazungumzia matumaini na changamoto za kura ya maoni iliyoanza jana huko Sudan ya Kusini, akisema kwamba uwezekano wa kuzaliwa taifa jipya katika Afrika upo wazi, lakini isitazamiwe kuwa mafanikio ya taifa hilo yatakuwa ya haraka haraka kiasi hicho.

Mhariri anasema kwamba, ni jambo linalofahamika, kwa watu wa Sudan ya Kusini kuwa na hamasa na hamu kubwa ya uhuru wao, hasa baada ya miaka ishirini ya vita na wenzao wa Kaskazini, ambavyo vilisababisha vifo vya zaidi ya watu milioni mbili wengine milioni nne kuwa wakimbizi. Lakini lazima pande zote mbili, Kusini na Kaskazini, zichukue tahadhari kubwa, hasa inapokuja fitina ya rasilimali ya mafuta.

Mhariri anamalizia kwa kusema, wakati Kusini wana mafuta kwenye ardhi yao, wa Kaskazini ndio wenye mabomba na mitambo ya kusafishia mafuta hayo. Lazima kati yao, kwa hivyo, pawe na biashara ya nipa-nikupe, tena si kwa dhamira ya kukomoana, bali ya kusaidiana.

Nayo tahriri ya gazeti la Ostsee, inazungumzia jaribio la mauaji dhidi ya Gabrielle Giffords, ambaye ni mjumbe katika Bunge la Marekani wa jimbo la Arizona kupitia chama cha Rais Barack Obama cha Democratic. Ijapokuwa Giffords hadi sasa anauguzwa hospitalini, wenzake sita waliuawa papo hapo.

Mhariri wa Ostsee Zeitung anasema kuwa, chuki na itikadi kali za kidini yanaweza kuwa mambo yaliyo nyuma ya shambulizi hili, na anaelekeza lawama zake za kwanza kwa chama cha kihafidhina, ambacho kimekuwa kikipata wafuasi wengi hivi karibuni, Tea Party.

Kwa msaada wa Sarah Palin, aliyewahi kuwa mgombea uteuzi wa chama cha Republican kwa ajili ya uchaguzi wa Rais wa Marekani, Tea Party kimeonesha namna watu wasiokuwa na uelewa mpana wa mambo wanavyoweza kuziharibu siasa na akili za vijana. Na tukio hili la mauaji ndiyo matokeo yake.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA

Mhariri: Josephat Charo