1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chuma cha Baghdadi kimotoni, Rex Tillerson

23 Machi 2017

Muungano wa mataifa dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS, unaoongozwa na Marekani, umeapa kuwaangamiza magaidi hao. Hayo yanafuatia  mkutano ulioandaliwa mjini Washington siku ya Jumatano.

https://p.dw.com/p/2Znoc
USA Anti-IS-Koalition in Washington
Wawakilishi wa mataifa 68 waliohudhuria mkutano wa Washington dhidi ya ISPicha: picture-alliance/AP Photo/C. Owen

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Rex Tillerson, aliwakaribisha mawaziri wenzake kutoka mataifa ya Kiarabu na nchi za Magharibi ambao ni wanachama wa muungano huo wa mataifa 68, akiahidi kiongozi wa IS Abu Bakr al-Baghdadi ataangamizwa.

Katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo, mataifa wanachama wa muungano huo walielezea azimio lao la kuongeza kasi ya juhudi za kuliangamiza kundi la IS nchini Iraq, Syria na katika mataifa mengine na yalipongeza hatua zilizopigwa na vikosi vya mataifa hayo katika ngome za IS katika mji wa Mosul ulioko kaskazini mwa Iraq na  mji wa Raqa nchini Syria.

Wakati wakitabiri ushindi katika mapambano hayo, waliapa pia kuwazuia wapiganaji wa kundi hilo la kigaidi wanaotoroka kueneza propaganda katika mtandao na kufanya hali kuwa tete.

Baghdadi ni lazima atauwawa pia

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson alisema lengo kuu la Marekani ni kulimaliza kundi la IS na viongozi wake.

Abu Bakr al-Baghdadi Führer Islamischer Staat
Kiongozi wa IS Abu Bakr al-BaghdadiPicha: Getty Images/AFP

"Karibu wasaidizi wote wa kiongozi wa IS Abu Bakr al-Baghdadi wameuwawa kwa sasa, wakiwemo wale wahusika wakuu wa mashambulizi ya Paris, Brussels na kwengineko. Ni suala la mda tu kabla Baghdadi mwenyewe hajapatikana katika hali sawa na hiyo," alisema waziri Rex Tillerson.

Afisa mmoja wa ulinzi wa Marekani aliwaambia wanahabari mwezi huu, Baghdadi ameutoroka mji wa Mosul, ambao umezungukwa na kikosi cha Iraq, na kwa sasa hana mawasiliano ya mara kwa mara kumuwezesha kuwaamrisha wapiganaji wake.

Miongoni mwa malengo ya muungano huo ni kuendelea kuwasaidia watu kurejea makwao na kushirikiana na viongozi wa kisiasa katika nchi hizo ili kudhibiti hali. Tillerson alisema hatua kama hizo zilifanikiwa nchini Iraq na kwa sasa muungano huo unapanga mikakati ya kufuata mkondo huo huo nchini Syria.

Nchi wanachama zimetoa zaidi ya Dola bilioni 20 kuunga mkono vita dhidi ya IS

"Kulipunguza makali kundi la IS sio lengo letu. Ni sharti tuliangamize kundi la IS. Natambua kwamba kuna masuala mengi muhimu Mashariki ya Kati, ila lengo la kwanza kwa Marekani ni kulishinda kundi hilo," alisema Tillerson, "kama tulivyosema hapo awali, ikiwa kila kitu ni muhimu, hakuna umuhimu wa kitu. Ni lazima tuweke fahamu zetu katika lile jambo la dharura lililoko mbele yetu."

Rex Tillerson Anti -IS- Koalition Washington
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Rex TillersonPicha: picture alliance/dpa/C. Owen

Wizara ya  mambo ya nchi za nje ya Marekani ilisema tangu kubuniwa kwa muungano huo wa mataifa 68 mwaka 2014, wanachama wake wametoa dola bilioni 22.2 kama fedha za misaada ya kibinadamu na usaidizi wa kiuchumi katika nchi za Iraq na Syria.

Waziri Tillerson alitangaza kwamba, wamekusanya zaidi ya lengo waliloliweka mwaka jana la dola bilioni 2.3 kwa ajili ya kuunga mkono vita hivyo dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu.

Mwandishi: Jacob Safari/AFP/DPA

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman