1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda chafungwa

2 Septemba 2011

Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda kimefungwa kwa kipindi kisichojulikana baada ya wahadhiri wa chuo hicho kugoma kufundisha, wakitaka nyongeza ya asilimia mia mia tatu na ishirini ya mshahara.

https://p.dw.com/p/12Rvk

Pia wanataka kurudishiwa fedha zao za akiba ya uzeeni ambazo walikuwa wanaweka kwenye kampuni ya bima ya National insurance corporation ambayo sasa imenunuliwa na serikali.


Chuo hicho, kimefungwa wiki mbili tu baada ya kufunguliwa kwa hula wa pili wa mwaka wa masomo. Wahadhiri wanasema bei ya bidhaa muhimu imekuwa ghali sana, hali inayowafanya wasiweze kumudu kutokana na mishahara wanayoipata.

Leylah Ndinda na ripoti kamili kutoka Kampala.

Kufungwa kwa chuo cha Makerere kulitangazwa na mwenyekiti wa baraza la
chuo daktari Charles Wana- Etyem baada ya baraza la chuo hicho na
waadhiri kutokubaliana ni vipi watautanzua mzozo huu. Waadhiri ambao wanataka asili mia mia tatu ishirini ya nyongeza ya mshahara wao walisema hawarudi darasani kabla ya kupata nyongeza hiyo.

Habari za kufungwa kwa chuo hiki zilipokelewa kwa hasira na wanafunzi:

Tumewakasirikia wale wote waliofanya uamuzi huu iwe baraza la chuo au waadhiri. Tumekasirika sana sana sana:

Watu wanaharibu muda mwingi hapa. Watu walikuja hapa kusoma lakini hawasomi. Hii ni shida kubwa sana. Wamesema tende nyumbani lakini kunao wanafunzi ambao hawana hata nauli ya kurudi nyumbani kwa hivyo ni shida kubwa.

Kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia mwaka wa elfu moja mia tisa tisini na sita wahadhiri walikuwa na akiba ya uzeeni waliochangia kila mwezi kwenye kampuni ya National insurance corporation kwa ufupi NIC iliyomilikiwa na raia wa Nigeria. Mwaka wa elfu mbili na tisa serikali iliinunua kampuni hii ya bima na sasa waadhiri wanataka serikali iwarejeshee pesa zao zipatao bilioni kumi na sita nukta saba pesa za Uganda .

Mhadhiri John Nzokwa akilizungumzia suala hili anasema

Akizungumzia kufungwa kwa chuo hiki mwenyekiti wa chama cha wa´hadhiri Prof Tanga Odoi alisema ni jambo la kusikitisha kuwa wahadhiri hawakuwa na imani kuwa serikali ilikuwa inatilia maanani ombi lao na ndio
wakaamua kutorudi darasani hata baada ya baraza la chuo cha Makerere ambalo linaawakilisha serikali kuwasihi warudi darasani na maombi yao yatashughulikiwa.

Wahadhiri hupata mshahara usiozidi dola mia saba pesa za marekani
lakini sasa wanasema wanataka mshahara usiopungua dola elfu nne.

Serikali inasema kiasi cha nyongeza wanachoitisha ni kikubwa sana
lakini mzazi mmoja ambaye mwanawe anasomea kwenye chuo cha Makerere anasema:

Hizo sio pesa nyingi. Ikiwa kuna pesa za kununua gesi ya kutoa
machozi na vinginevyo, kwa nini wasiwalipe walimu

Wiki iliyopita serikali ilisema haiwezi kuwaongeza wahadhiri mshahara peke yao lakini watawaongeza mshahara wafanyikazi wote wa serikali mwaka wa fedha ujao.

Mwandishi: Leylah Ndinda

Mhariri. Miraji Othman