1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton ahitimisha ziara yake Afrika

Kabogo Grace Patricia14 Agosti 2009

Kituo cha saba na cha mwisho cha ziara yake hiyo ni Cape Verde

https://p.dw.com/p/J9uJ
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Rodham Clinton, (Kati) na Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, (Shoto) wakiwa na Mkuu wa Polisi wa Liberia, Marc Armblah.Picha: AP

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton leo anamaliza ziara yake katika mataifa saba barani Afrika kwa kuzuru Cape Verde. Bibi Clinton yuko katika siku yake ya mwisho ya ziara ya siku 11 iliyokuwa na lengo la kuonyesha jinsi serikali ya Rais Barack Obama wa Marekani inavyozingatia umuhimu wa bara la Afrika kwa kulitaka liwe na utawala bora.

Bibi Clinton amesema anaamini ziara yake imekuwa na mafanikio na imesaidia kujenga mahusiano imara baina ya Marekani na Afrika. Akizungumza jana baada ya kukutana na Rais Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia, Bibi Clinton alisema ziara hiyo ni muhimu sana kwake na Rais Obama, iliyopeleka ujumbe wa kuonyesha jinsi nchi hiyo inavyotaka kuimarisha uhusiano na bara la Afrika, siyo tu kwa serikali za bara hilo, bali pia wananchi wenyewe wa Afrika. Akigusia hotuba iliyotolewa na Rais Obama katika ziara yake nchini Ghana, Bibi Clinton alisema:

''Rais anajichukulia mwenyewe kama mtoto wa Afrika na katika hotuba yake aliyoitoa Ghana, alisema matumaini yake mengi na nini kilicho ndani ya moyo wake. Alisema maisha ya baadaye ya Afrika yako mikononi mwa Waafrika wenyewe na maisha ya Liberia yako kwa Waliberia wenyewe.''

Kabla ya kurejea mjini Washington baadaye hii leo, Bibi Clinton anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Cape Verde, Jose Maria Neves, nchi ambayo maafisa wa Marekani wameipongeza kwa kutumia vizuri msaada wa kiuchumi wanaopewa na Marekani. Nchi hiyo ni ya kwanza kwa kutumia vizuri msaada wa Millenium Challenge Corporation uliotolewa na Marekani. Kwa mujibu wa maafisa hao wa Marekani, nchi hiyo inatoa fedha kwa nchi zinazoheshimu demokrasia na utawala bora. Chini ya mpango huo, Cape Verde ilisaini msaada wa dola milioni 110 mwaka 2005 kwa ajili ya kuimarisha uchumi wake, ikiwemo miradi mbalimbali ya miundombinu na uwekezaji katika kilimo.

Katika ziara yake hiyo ya mataifa saba, Bibi Clinton amezitaka serikali za mataifa hayo kumaliza tatizo la rushwa, kuimarisha demokrasia na kuzingatia kuheshimu haki za binaadamu, hasa haki za wanawake.

''Changamoto kwa kila serikali yenye kuheshimu demokrasia, iwe ya miaka mitatu au miaka 233 kama ya kwetu ni jinsi ya kuelezea athari hizo katika matokeo na maisha ya watu.''

Waziri huyo wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani amezitembelea pia nchi za Kenya, Afrika Kusini, Angola, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Nigeria, Liberia na Cape Verde. Hii ni ziara ndefu kufanywa na Bibi Clinton tangu aliposhika rasmi wadhifa huo mwezi Januari, mwaka huu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/AFPE)

Mhariri: M. Abdul-Rahman