1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hillary Clinton: Nataka kuwa rais

13 Aprili 2015

Hillary Rodham Clinton amejitosa tena katika siasa za urais wa Marekani mwaka 2016, kwa ahadi ya kuwa kinara wa Wamarekani wa kawaida katika taifa ambako ukosefu wa usawa wa kipato unazidi kutanuka.

https://p.dw.com/p/1F6mq
Hillary Clinton
Picha: Kamm/AFP/Getty Images

Tofauti na miaka nane iliyopita wakati alipogombea na kushindwa na Barack Obama, Clinton na historia yake binafasi hawakuwa fokasi ya ujumbe wake wa kwanza wa kampeni. Hakuzungumzia wakati wake katika baraza la Seneti wala miaka yake minne kama waziri wa mambo ya kigeni, au uwezekano wake wa kuandika historia kama rais wa kwanza mwanamke kuiongoza Marekani.

Badala yake, video yake ni mkusanyiko wa wapigakura wanaozungumzia maisha yao, mipango yao na matarajio yao ya baadae. "Wamerekani wamepambana kutoka katika nyakati ngumu za kiuchumi, lakini hali iliyopo bado inaendelea kuwanufaisha wale walioko juu. Wamarekani wa kawaida wanahitaji kinara, na nahitaji kuwa kinara huyo," Clinton alisema mwoshoni mwa video ya tangazo lake.

Obama na Clinton wakiwa bado maseneta mwaka 2007.
Obama na Clinton wakiwa bado maseneta mwaka 2007.Picha: Reuters/Larry Downing

Video hiyo ya Clinton pamoja na mtandao wake havikugusia masuala ya kisera hasa. Lakini ujumbe huo ulinuwiwa kuwavutia Waliberali wa chama cha Democrats, ambao wanachukulia usawa wa kiuchumi kama suala la kipaumbele.

Kutilia mkazo Iowa, New Hampshire

Clinton sasa anapanga kuelekea katika majimbo yenye maamuzi ya Iowa na New Hampshire, kuungana na wapigakura. Clinton anatumai kuepusha makosa ya mwaka 2008, alipoingia kinyanganyiro hicho kama mgombea anaepewa nafasi kubwa zaidi ya kushinda, na kushangazwa na Obama katika jimbo la Iowa.

Clinton mwenye umri wa miaka 67 anaingia katika kinyanganyiro hicho akiwa na rekodi ndefu ya utumishi wa umma, historia itakayomsaidia na pia kumuumiza. Tayari wagombea wa chama cha Republican walikuwa wanaanda ujumbe utakaomhusisha kashfa za mihula miwili ya utawala wa mume wake Bill Clinton katika miaka ya 1990.

Kwa kulielewa hilo, wafanyakazi wake wamesema anapanga kujitanabaisha kama "mpiganaji shupavu" aliedhamiria kuzuwia nguvu inayozidi kukuwa ya chama cha mrengo wa kulia cha Republican, ambacho kimetaka kuvuruga ajenda ya Obama, na sasa kinadhibiti mabaraza yote mawili ya bunge la Congress. Obama alisema siku ya Jumamosi kwamba anadhani Clinton atakuwa rais bora.

Clinton anaingia kinyanganyiro hicho wakati ambapo uchunguzi wa maoni unamuonyesha akiwa na nafasi nzuri zaidi ya kumrithi Obama. Hata hivyo, katika kipindi cha nusu karne iliyopita, chama kimoja kimeshika ikulu kwa mihula mitatu mfufulizo mara moja tu, wakati wa tawala za Warepublican Ronald Reagan na George H.W. Bush.

Clinton akiwa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani huko nyuma.
Clinton akiwa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani huko nyuma.Picha: imago/Jens Schicke

Republicans wapanga mashambulizi

Warepublican watajaribu kukabiliana na nguvu ya Clinton kwa kumuonyesha kama mtu asiyeaminika. Wamemtuhumu kwa kutumia akaunti binafasi ya barua pepe pamoja na "server" iliyoko nyumbani kwake badala ya kutumia vya serikali wakati alipokuwa waziri wa mambo ya kigeni.

Pia wameibua maswali juu ufadhili kutoka serikali za kigeni kwa wakfu wa familia ya Clinton. Mwenyekiti wa chama cha Republican Reince Priebus, alisema kuchaguliwa kwa Clinton itakuwa sawa na kumpa Obama "mhula wa tatu." Baadhi ya Warepublican pia wanataka kuifanya sera ya kigeni kuwa suala kuu wakati ambapo utawala wa Obama unajadiliana makubaliano ya nyuklia na Iran, na kuchukuwa hatua kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Cuba.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,afpe,rtre.
Mhariri: Daniel Gakuba