1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton amkabidhi Obama ripoti ya juhudi za amani Mashariki ya kati

23 Oktoba 2009

Asema kuna maendeleo fulani bado kuna kazi kubwa.

https://p.dw.com/p/KDbh
Bibi Clinton na Rais Obama.Picha: AP

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton amemkabidhi rais wake Barack Obama ripoti juu ya juhudi za utawala wake hadi sasa za kujaribu kuleta makubaliano ya amani katika Mashariki ya kati kati ya Israel na Wapalestina.

Bibi Clinton alionana na rais Obama Ikulu mjini Washington na kumkabidhi ripoti hiyo muhimu kuhusu maendeleo yaliofikiwa hadi sasa na ujumbe wa Obama ili kuleta makubaliano kati ya Israel na wapalestina na kuepusha hali mpya ya mkwamo.

Rais Obama amelipa kipa umbele suala hilo katika sera yake ya mambo ya nchi za nje na kuwashawishi Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na rais wa Palestina Mahmoud Abbas , wajiunge naye kwa mkutano wa kilele mwezi uliopita, uliofanyika mjini New York.

Lakini licha ya juhudi za Obama, Clinton na mjumbe maalum katika Mashariki ya kati George Mitchell bado njia ya kufikia lengo hilo hajafikiwa kukiwa bado na mvutano kati ya pande husika. Kwa mujibu wa afisa mmoja wa utawala wa Obama ,katika ripoti ya Bibi Clinton, waziri huyo wa kigeni amemshauri rais Obama akisema kwamba changamoto bado ingalipo wakati Marekani ikiendelea kuzungumza na pande zote mbili ili kuyafufua mazungumzo ya amani katika mazingira ambayo yataweza kuleta mafanikio.

George Mitchell
Mjumbe wa Obama Mashariki ya kati,Seneta wa zamani George Michell.Picha: picture alliance / landov

Afisa huyo ambaye hakutaka kutajwa jina akasema ,bibi Clinton alisisitiza hata hivyo kuwa kuna maendeleo fulani yaliopatikana, lakini pande mbili husika Israel na Wapalestina zinapasawa kufanya jitihada kubwa zaidi kwa upande wao na kuongeza kwamba Wapalestina wameimarisha juhudi zao katika suala la usalama na kuzifanyia mageuzi taasisi zao lakini bado kunahitajika juhudi za ziada katika nyanja nyengine na kuzuwia uchochezi na ugaidi.

Kwa upande wa Israel ripoti hiyo inasemekana kutaja kwamba dola hiyo ya Kiyahudi imeruhusu nafasi kubwa zaidi ya nyendo za wapalestina na kujibu wito wa kuitaka izuwie shughuli za ujenzi wa makaazi ya walowezi, kwa kuonyesha kuwa tayari kupunguza shughuli hizo.

Lakini Waisraili kwa mujibu wa afisa aliyezungumzia ripoti hiyo wanapaswa kuchukua hatua za kivitendo na juhudi zaidi kuboresha hali za kila siku za maisha ya wapalestina, huku pande zote mbili zikihitaji kusonga mbele na kuwa na mazungumzo ya ana kwa ana.

Rais Obama amekua akijaribu kuitaka serikali ya waziri mkuu Netanyahu kuzuwia kabisa kuatanuliwa kawa makaazi ya walowezi ya kiyahudi katika eneo linalokaliwa la ukingo wa magharibi, na kuwataka Wapalestina wachukuwe hatua kuboresha usalama wa Israel.

Taarifa inasema mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya kati Bw Mitchell atarudi katika eneo hilo mnamo siku za usoni kuendelea na mazungumzo, wakati Waziri Clinton atashauriana na mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi za kiarabu nchini Mrocco tarehe 2 na 3 mwezi ujao wa Novemba.

Mwandishi:M.Abdul-Rahman/AFP Mhariri: Josephat Charo