1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton apata wajumbe wa kutosha kuwa mgombea

Mohammed Khelef7 Juni 2016

Hillary Clinton amepata ahadi za wajumbe wa kutosha kuweza kumfanya kuwa mgombea wa urais wa Marekani kwa chama cha Democrat, kwa mujibu wa hisabu iliyochapishwa na shirika la habari la Associated Press (AP).

https://p.dw.com/p/1J1hG
Mgombea uteuzi wa kugombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Democrat, Hillary Clinton.
Mgombea uteuzi wa kugombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Democrat, Hillary Clinton.Picha: pictue-alliance/epa/P. Buck

Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje anaripotiwa kuifikia idadi inayotakiwa ya wajumbe, ikiwa ni siku moja kabla ya majimbo sita, likiwemo la Carlifornia, kufanya kura za mchujo hivi leo, na ikiwa ni miaka minane tangu kushindwa na rais wa sasa, Barack Obama.

Mwenyewe Clinton yuko kwenye jimbo hilo la Carlifornia akiendeleza kampeni za usiku kucha, kuwaomba wajumbe wazidi kujitokeza kumpigia kura, hata baada ya matokeo hayo kuchapishwa na AP.

"Ni jambo kubwa kwa California kupiga kura kwani Carlifornia ndio mustakabali wetu. Ndiyo itakayotusaidia kutengeneza mustakabali tuutakao kwa kila mtu wa nchi hii. Na tutamaliza kura kura za mchujo tukiwa imara zaidi kuweza kumuangusha Donald Trump." Aliwaambia wafuasi wake.

Rais Obama, ambaye alimshinda Clinton kwenye kinyang'anyiro cha mwaka 2008 kuwania uteuzi wa Democrat, anajitayarisha kumuidhinisha rasmi waziri wake huyo wa zamani, na kuanza kampeni kubwa na za waziwazi kumpinga Trump. Ikulu ya Marekani inasema tangazo hilo litatolewa hivi karibuni, ingawa haiwezi kuwa kabla ya kura za usiku wa leo.

Juzi Jumapili, Obama alimpigia simu hasimu wa Clinton, Bernie Sanders, wakati mgombea huyo akiwa kwenye kampeni za Carlifornia, ingawa hakuna mengi yaliyosemwa kuhusu mazungumzo ya wawili hao.

Mgombea uteuzi wa kugombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Democrat, Barnie Sanders.
Mgombea uteuzi wa kugombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Democrat, Barnie Sanders.Picha: picture-alliance/AP Photo/D. Dovarganes

Sanders ashikilia kusalia kwenye kinyang'anyiro

Hata hivyo, Sanders amesisitiza kuwa Clinton hajafikia nafasi ya kuwa mgombea rasmi wa Democrat na kwamba ni wajumbe wakuu wa chama chao tu watakaoamua hilo, jambo ambalo litafanyika kwenye mkutano mkuu wa mwezi Julai.

Msemaji wa Sanders, Michael Briggs, amesema ni bahati mbaya kuwa vyombo vya habari vimefikia hitimisho, ilhali muda haujawadia. Sanders anasema ana matumaini ya kuweza kuwashawishi wajumbe wa mkutano huo mkuu kuwa ni yeye peke yake mwenye uwezo wa kupambana na mgombea mtarajiwa wa Republican, Donald Trump.

"Sipo hapa kuukana ukweli hata kidogo, lakini tutakwenda kuhoji mbele ya wajumbe wakuu na kila mtu kwenye Mkutano Mkuu wa Democrat atataka kumshinda Donald Trump kwa sababu moja tu nzuri, nayo ni kuwa yeye ni janga na hapaswi kuwa rais wa Marekani. Na kwa mujibu wa kila mtu ni kuwa ni Bernie Sanders ni mgombea madhubuti zaidi dhidi ya Trump kuliko Hillary Clinton," alisema mgombea huyo kwenye mazungumzo yake na mwandishi wa AP.

Licha ya kile kinachoonekana kuwa ushindi wa wazi wa Clinton kwenye kinyang'anyiro hiki, endapo Sanders atashinda jimbo la Carlifornia anaweza kuyumbisha maoni ya wajumbe wakuu na tayari wafuasi wake wamesema wataendelea kumpigania mgombea wao hadi dakika ya mwisho.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga