1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton kukutana na Rais wa Somalia leo.

Halima Nyanza6 Agosti 2009

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton ambaye yupo nchini Kenya ikiwa ni sehemu ya ziara yake ndefu barani Afrika, anakutana leo mjini Nairobi na Rais wa serikali ya mpito ya Somalia.

https://p.dw.com/p/J4cE
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hilary Clinton akihutubia mkutano wa AGOA, mjini Nairobi na leo pia atakutana na Rais wa serikali ya mpito ya Somalia.Picha: picture alliance / dpa

Mapema kabla ya mkutano wake na Rais wa mpito wa Somalia, Bibi Clinton aliweka shada la maua katika eneo lilikotokea shambulio la bomu dhidi ya Ubalozi wa Marekani mjini Nairobi mwaka 1998, ambapo watu 213 waliuawa.

Waziri huyo wa kigeni wa Marekani alisema hii ni nafasi ya kufanya tena maamuzi upya na kuhakikisha kuwa tunafanya kila linavyowezekana ili mashambulio kama hayo hayatokeo na kuua watu wasio na hatia.

Bibi Clinton pia atakutana baadaye na rais huyo wa Somalia, ambaye Marekani inaamini kuwa ni tumaini nzuri katika kuimarisha nchi hiyo iliyokumbwa na vita kwa karibu miongo miwili sasa.

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani amewaambia Waandishi wa Habari kwamba, atazungumza na Rais huyo wa Somalia juu ya nini Jumuia ya Kimataifa itafanya kujaribu kuunga mkono juhudi za kiongozi huyo kuimarisha Somalia na kuunda serikali.

kutokana na kwamba hali iliyoko sasa nchini humo ni tishio kwa Kenya pamoja na kuwa kitisho katika kuimarisha bara zima la Afrika na nje ya bara hilo.

Aidha Bibi Clinton amekiri kuwa mzozo wa kisiasa nchini Somalia ni mgumu zaidi kutokana na kuwepo kwa dalili za ugaidi ndani ya nchi hiyo.

Ametolea mfano kundi la Al Shabaab linalopigana nchini Somalia ambalo linadaiwa kuwa na uhusiano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda, pamoja na vikundi vingine vya wapiganaji wenye msimamo mkali ambavyo ni tishio kwa serikali ya Rais Sheikh Sharif.

Naye Msaidizi wa Bibi Clinton katika masuala ya Afrika Johnnie Carson amesema Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani yuko tayari kutoa misaada mingine kwa serikali hiyo ya mpito.

Marekani pia na washirika wake wamekuwa waiituhumu Eritrea kuchochea mapigano nchini Somalia.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa aliiionya Eritrea wiki iliyopita, kuacha tabia yake hiyo vinginevyo itaadhibiwa na Marekani ikiwemo uwezekano wa kuwekewa vikwazo.

Watafiti wa Mambo wanahofu kwamba Somalia inaweza kugeuka kuwa makazi ya makundi yenye uhusiano na mtandao wa Al Qaeda iwapo Rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed kama hatapewa nguvu zaidi na washirika wake wa nje.

Somalia ni nchi ambayo imepewa kipaumbele katika ziara hiyo ya bibi Clinton.

Akiwa nchini Kenya Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje amekutana pia na viongozi wa serikali ya nchi hiyo na kuwataka kuharakisha kutekeleza marekebisho kadhaa katika juhudi za kupambana na rushwa na uvunjifu wa haki za binadamu.

Kenia USA Außenministerin Hillary Clinton in Nairobi
Bibi Clinton kushoto akiwa na Rais wa Kenya kulia kabisa mjini Nairobi.Picha: AP

Katika hatua nyingine Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani anatarajiwa kuzungumza na wanafunzi kabla ya kuondoka baadaye leo kuelekea Afrika kusini, kituo chake cha pili katika ziara yake ya kuyatembelea mataifa saba ya Afrika, ziara ambayo ni ndefu kuifanya tangu kuchaguliwa kwake kama Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani.

Mwandishi: Halima Nyanza(AFP)

Mhariri:M. Abdul-Rahman