1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton na Trump wamsifia Merkel

30 Septemba 2016

Mgombea wa Urais wa Marekani Donald Trump amegeuka na kuanza kumsifu Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kuwa ni mfano bora katika maswala ya uongozi, baada ya kumlaumu kiongozi huyo kwa miezi kadhaa.

https://p.dw.com/p/2Qlf4
Angela Merkel na Donald Trump (picture alliance )

Trump alikuwa akimlaumu Merkel kwa kuiharibu Ujerumani kutokana na sera yake ya kuwaruhusu wakimbizi kutoka Syria kuingia nchini humo. Donald Trump, mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha Republican nchini Marekani alijibu pale alipoulizwa kwenye mahojiano na gazeti la New England kuhusu ni nani anayefikiria kuwa ni kiongozi bora zaidi ulimwenguni? Ndipo alipojibu kuwa anafikiri Kansela wa Ujerumani  Angela Merkel  ndiye haswa kiongozi mwenye sifa za uongozi bora duniani kote.  Hata hivyo bado alisisitiza lawama zake kwa bibi Merkel juu ya uamuzi aliyoufanya kuhusu uhamiaji.  

Sifa hizo kwa Kansela wa Ujerumani zimewakutanisha wagombea wawili wa Marekani Hillary Clinton na Donald Trump wote wakiwa wanamwagia sifa Angela Merkel na  kuwafanya japo kwa mara moja wawe wanakubaliana katika jambo.

Lawama kwenye kampeni ya Urais Marekani

Hillary Clinton
Hillary Clinton atapambana na Trump katika uchaguzi mkuu Novemba 8Picha: Reuters/A. Latif

Wakati huo huo viongozi hao wawili wa Marekani wameendelea kutupiana lawama katika kampeni zao. Hillary Clinton amesema ripoti mpya iliyotolewa inaonyesha kuwa huenda mgombea huyo  mwenza wa urais akawa amekiuka sheria ya Marekani kuhusu vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Cuba, Clinton anasema huo ni ushahidi tosha  kuonyesha ni jinsi gani Trump anavyoweka mbele maslahi yake binafsi pamoja na biashara yake kuliko yale ya taifa la Marekani. 

Gazeti la Newsweek limeripoti juu Trump kuilipa kampuni ya ushauri kiasi cha dola elfu 68 za Kimarekani kama gharama za bishara katika hoteli zake na majumba ya starehe na kucheza kamari huko Cuba. Trump na kampuni hiyo hazikutafuta ruhusa ya serikali kabla kuendelea na biashara hiyo.

Kwa upande wake Donald Trump anakumbushia kesi ya utovu wa nidhamu iliyowahi kumkabili aliyekuwa rais wa Marekan Bill Clinton na kuwakumbusha Wamarekani kuwa familia hiyo si watu wasafi kitabia. Trump aliuambia umati wa watu kwenye kampeni yake katika mji wa Bedford huko New Hampshire kwamba wanapaswa wakumbuke mwaka1998 pale bunge la Marekani lilipomuhukumu Bill Clinton kwa kutumia madaraka vibaya, kusema uongo na kuzuia haki. hivyo basi anmuunganisha Hillary Clinton na makosa ya mumewe. Bill Clinton lakini alivuliwa mashtaka hayo na bunge la Seneti.

Kuhusu mauaji ya mtu mmoja mwenye asili ya Kiafrika aliyeuwawa na na polisi katika mji wa Charlotteulio katika jimbo la North Carolina, pamoja na matokeo ya baada ya mauaji hayo, wote wawili Clinton na Trump wemeendeleza siasa za kuwagawanya watu katika kampeni zao za kutafuta wapiga kura zaidi.

Vyama vyote viwili Republicans na Democrats vinasema mauaji ya Keith Lamont Scott yataendelea kuleta msisimko kwa wafuasi wao katika kinyang'anyiro hicho cha kumtafuta atakaye kuwa rais mpya wa Marekani baada ya rais Barack Obama.    

Mwandishi: Zainab Aziz/APE

Mhariri: Yusuf Saumu