1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Col. Bacar akimbilia Reunion ?

27 Machi 2008

Col.muasi wa Nzouani M.Bacar ameomba hifadhi ya kisiasa Ufaransa na amekimbilia Mayotte.

https://p.dw.com/p/DVlO
Wanajeshi wa nje wakishangiliwa kisiwani AnjouanPicha: AP

Col.Mohammed Bacar,kiongozi-muasi wa Nzouani,mojwapo ya visiwa vya Comoro, ameomba hifadhi ya kisiasa nchini Ufaransa ambayo inapanga kumsafirisha katika kisiwa cha Reunion-si mbali na Mayotte baada ya wanzouni waishio Mayotte kupinga kuwapo kwake huko.

Mayotte, hadi Comoro ilipojitangazia uhuru kutoka Ufaransa 1975,kilikuwa kisiwa cha 4 cha Comoro. Maandamano ya wacomoro hadi 700 yalifanyika leo mmjini mbele ya Ubalozi wa Ufaransa mjini Moroni kulalamika kwa jinsi Ufaransa inavyoingilia maswali ya Comoro.

Waziri mdogo wa Ufaransa wa maswali ya n'gambo Yves Jego amearifu leo kuwa Col. Bacar amewekwa kizuizini uwanja wa ndege wa Mayotte akisubiri kusafirishwa hadi (La Reunion) au Reunion. Akasema atasikilizwa maombi yake halafu Ufaransa itaamua hatima yake.

Wanajeshi wa Ufaransa wanatazamiwa kumsafirisha Col.Bakari hadi Reunion.Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Ufaransa Laurent Teisseire, amesema milki ya ngambo ya Ufaransa ya Reunion,imekubali kumpokea Col.Bacar na imewataka maafisa wa kijeshi wa kifaransa kumpeleka huko.

Akaongeza,

" watawala wa Mayotte wanahisi ni vyema Bacar na wenzake aliotorokanao hawabaki Mayotte kutokana na kuwapo kwa wanzuoani wengi kisiwani humo."

Wacomoro waishio n'gambo Mayotte, waliaandamana kwa hasira kupinga kuwapo kwa col.Bacar kisiwani Mayotte alikokimbilia jana kwa marekebu ya mwendo wa kasi mno kutoka Nzouani baada ya majeshi ya Comoro yakisaidiwa na yale ya Tanzania na Sudan, kumtimua Nzouani.

Vikosi vya nchi za kiafrika na vile vya Comoro vinasimamia ulinzi kisiwani nzouani wakati huu.

Serikali ya Comoro imeitaka Ufaransa kumrejesha Comoro Col.Bacar kukabili mashtaka.

Wakati hatima ya kiongozi-muasi Mohammed Bacar iko mikononi mwa Ufaransa ,serikali ya Moroni,kisiwani Ngazija,imemteua makamo-rais Ikililou Dhoinine kuongoza ujumbe wa serikali kuu ya shirikisho huko Anzouani hadi pale serikali ya mpito itakapoweza kuundwa-alisema waziri wa Baraza la mawaziri Ali Mmadi.Serikali ya mpito ya Nzouani, yatarajiwa kuundwa mwishoni mwa wiki hii na Baraza lake jipya latazamiwa kutangazwa kesho ijumaa.

Bw.Mmadi amearifu serikali hiyo ya mpito itaongozwa na Mkuu wa Mahkama ya rufaa ya Nzouani ,Laili Zamane na uchaguzi mpya utafanyika mwezi Mei.

Majeshi ya Tanzania,Sudan na ya Comoro, yalishangiriwa kwa shangwe na wakaazi wa Nzouani yalipoingia huko jana yakikabili upinzani mdogo tu kutoka kwa wapiganaji wa Col.Bacar.

Wakosoaji wanadai, UA umechagua shabaha hafifu kulenga hujuma zao.Comoro binafsi, imevunjwa moyo na rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini kwa kupinga matumizi ya nguvu kisiwani Nzouani.Mbeki alietembelewa wiki chache nyuma na rais Nicolai Sarkozy wa Ufaransa.Huko rais wa Sarkozy, alinadi kudurusu siasa za ulinzi za Ufaransa na makoloni yake ya zamani ya Afrika.Iwapo hii itajumuisha Comoro na Mayotte,yafaa kusubiri kuona.

Kikundi cha UA cha mawasiliano juu ya mzozo wa Comoro kimejumuisha Afrika Kusini,Tanzania ,Sudan,Senegal na Libya.