1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Madhara ya kukwama kwa makubaliano ya amani Colombia

6 Oktoba 2016

Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa unaweza kusitisha kutoa fedha za maendeleo ambazo zilitengwa kwa ajili ya kuisaidia Colombia kufuatia kukwama kwa juhudi za kusitisha mapigano yaliyodumu kwa nusu karne.

https://p.dw.com/p/2QwGw
Kolumbien Juan Manuel Santos und Alvaro Uribe
Picha: Picture-Alliance/E. Herrera/Colombia's presidencial press office

Pesa hizo ambazo ni kiasi cha karibu euro milion 600 zilitengwa kwa ajili ya kuisaidia serikali mjini Bogota kusitisha mapigano ambayo yamedumu kwa nusu karne, na kuangamiza maisha ya baadhi ya watu. Kwa zaidi ya saa nne Rais Santos kwa nyakati tofauti alikutana na maraisi wa zamani Andres Pastrana na Alvaro Uribe kujadili hoja ambazo zimesababisha kukataliwa kwa makubaliano hayo ya amani ambayo yamesainiwa na Rais Santos pamoja na waasi wa FARC

Pastrana na Uribe wanataka kufanyika kwa mabadiliko katika makubaliano hayo wakisisitiza masharti magumu kwa waasi wa FARC, ambao makubaliano ya sasa yanawahakikishia nafasi 10 katika bunge na kupunguziwa vifungo kwa wapiganaji watakaokiri makosa yao.

"Tunaweka wazi mabadiliko ya awali ambayo ni lazima yazingatiwe na kutambulishwa katika makubaliano mapya ya amani ya havana ambayo yana uhusiano wa moja kwa moja na watu wa Colombia" alisema Alvaro Uribe

Uribe, ambaye chama chake cha democratic centre kiliongoza wapinzani katika kukataa makubaliano hayo, alisema baada ya kikao kuwa amani kwa wote ni bora kuliko makubaliano yasiyo na umakini kwa wachache.

Baadhi ya raia wa Colombia katika maandamano ya amani
Baadhi ya raia wa Colombia katika maandamano ya amaniPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Vergara

Wakati huo huo usiku wa Jumatano katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu wa nchi hiyo, maelfu ya raia wa Colombia wamefanya maandamano ya amani ambayo yameandaliwa na mitandao ya kijamii, makundi ya wanafunzi pamoja na makundi ya kijamii, wengi wakipeperusha bendera, wengine wakiwa na mishumaa na wengine wakiwa na picha za wapendwa wao ambao wameuwawa katika kipindi cha mapigano

Mmoja kati ya waandamanaji hao alisema "tunachoomba ni kuwa mchakato wa amani uharakishwe, makubaliano ya sasa tayari yana kasoro, tunataka amani ambayo haina siasa".

Maandamano hayo yanashinikiza mfumo wa siasa pamoja na waasi kutokata tamaa ya mkataba huo wa amani ambao umepingwa kwa tofauti ya kura chache sana, waliopinga ni asilimia 50.2 na waliounga mkono wakiwa ni asilimia 49.8

Mwandishi: Celina Mwakabwale/DPA/AP/AFP

Mhariri:Iddi Ssessanga