1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Colombia waukataa mkataba wa amani na FARC

Mohammed Khelef
3 Oktoba 2016

Wapigakura nchini Colombia wameyakataa makubaliano ya kihistoria ya amani kati ya serikali ya nchi yao na kundi la waasi la FARC katika matokeo yanayotajwa kuwashituwa wengi duniani kote.

https://p.dw.com/p/2Qoyp
Kolumbien Referendum gescheitert
Picha: picture alliance/AP Photo/A. Cubillos

Dunia imeshitushwa na matokeo ya kura ya maoni nchini Colombia, ambako wapigakura wameukataa mkataba wa amani kati ya serikali na kundi la waasi la FARC uliokusudia kukomesha zaidi ya nusu karne ya mapigano yaliyoangamiza maisha ya zaidi ya watu 260,000 na kuwahamisha kutoka makaazi yao wengine milioni saba, ingawa rais wa nchi hiyo na mkuu wa kundi la FARC wanasema bado wamedhamiria kusaka amani kwa kila hali. 

Inaonekana kama kwamba wapenda amani ndani na nje ya Colombia walishajiamulia kuwa wapigakura wasingeliweza kuyakataa makubaliano haya, na sasa baada ya kuyakataa, kauli za lawama zimekuwa zikitoka kila upande. 

Norway, taifa ambalo pamoja na Cuba, ilianzisha mazungumzo ya miaka minne kati ya serikali na waasi wa FARC imesema "imevunjwa moyo sana" na uamuzi huo wa wapigakura wa Colombia, licha ya kwamba ulipita kwa ushindi mdogo. Asilimia 50.2 iliamua kwamba makubaliano hayo hayahitajiki kwa sasa, huku asilimia 49.8 wakiyaunga mkono.

Kuba Timoshenko verfolgt den Ausgang des Referendums
Kiongozi wa waasi wa FARC, Rodrigo Londono, mashuhuri kwa jina la Timoleon Jimenez Timoshenko.Picha: picture alliance/dpa/E. Mastrascusa

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Borge Brende, amesema nchi yake itaendelea kuunga mkono jitihada za amani, na kwamba ujumbe wa wanadiplomasia kutoka nchi hiyo uko njiani kuelekea Havana, Cuba, kwahala ambako kumekuwa yakifanyika majadiliano kwa miaka kadhaa sasa.

Santos, Londono waapa kuendelea kusaka amani

Kauli ya kutia moyo katikati ya hisia za kushindwa imetolewa pia na Rais Juan Manuel Santos wa Colombia, ambaye akikiri kushindwa kwa kampeni yake ya ndio, ameapa kwamba kamwe hatokaa kitako hadi amani kamili ipatikane.

"Nazungumza nikiwa rais wa wale waliosema ndiyo kwa makubaliano ya amani na kwa wale waliosema hapana. Sijavunjika moyo. Nitaendelea kusaka amani hadi mwisho wa muhula wangu madarakani, maana mimi ndiye niliyepewa dhamana ya kuhakikisha usalama wenu," alisema Rais Santos kwenye hotuba yake kwa taifa.

Kolumbien Friedensvertrag mit Farc mit knapper Mehrheit abgelehnt
Rais Juan Maneul Santos akihutubia taifa baada ya kushindwa kwenye kura ya maoni.Picha: picture alliance/dpa/Presidency of Colombia

Kiongozi wa kundi la FARC, ambaye anaishi uhamishoni nchini Cuba, Rodrigo Londono, alisema mara baada ya matokeo hayo kutangazwa kwamba licha ya kuvunjika kwake moyo, bado FARC inaamini kuwa njia ya mazungumzo ndiyo pekee ya kupata suluhisho. 

"FARC inasikitika sana kwamba nguvu za maharibiko za wale wanaopandikiza chuki na visasi zimeathiri mawazo ya watu wa Colombia. Lakini tutatumia maneno na sio tena silaha kusaka amani hadi ipatikane."

Kwa kusema watu waliopandikiza chuki na visasi, Londono alikuwa akimaanisha timu ya hapana kwenye kampeni za kura hiyo ya maoni, ambayo iliongozwa na mwanasiasa wa upinzani mwenyu nguvu, rais wa zamani wa Colombia, Alvaro Uribe, ambaye naye baada ya matokeo hayo alisema hakuna asiyetaka amani, bali wanataka makubaliano ambayo hayatoi nafasi ya kuwapa utukufu waliolitendea makosa taifa hilo la Amerika Kusini.

Kushindwa huku kwa serikali ya Santos na waasi kwenye kura ya maoni kumepelekea mshituko mkubwa kwa wengi walioyaunga mkono makubaliano hayo, wakiwemo viongozi kadhaa wa kigeni.

Wakuu wengi wa mataifa na pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, walikuwepo wakati Santos na Londono wakiwema saini makubaliano hayo wiki moja iliyopita, katika sherehe iliyokuwa na hisia kali.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga