1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Colombia yaibwaga Cote d'Ivoire

20 Juni 2014

Mchezo mwingine wa kusisimua kutoka kwa James Rodriguez ambaye alifunga goli moja na kutengeneza jingine uliisaidia Colomboa kuwashinda Cote d'Ivoire magoli 2-1 katika mechi ya kundi C na kutinga awamu ya 16

https://p.dw.com/p/1CMZK
Fifa WM 2014 Elfenbeinküste Kolumbien
Picha: AFP/Getty Images

Rodriguez alifunga goli lake la pili katika dimba hilo, naye mchezaji aliyeingia kama nguvu mpya Juan Fernando Quintero, akafunga goli lake la kwanza la kimataifa, katika kipindi cha pili, kabla ya Gervinho kuonyesha umahiri wa kibinafsi kwa kuifungia Cote d'ivoire goli safi, lake la pili katika fainali hizo.

Colombia ambao wamecheza kwa mara ya kwanza katika Kombe la Dunia baada ya fainali za mwaka wa 1998, wamefuzu katika duru ya pili baada ya Japan na Ugiriki kutoka sare katika mechi nyingine iliyochezwa leo ya kundi C. Cote d'Ivoire bado wana nafasi ya kufuzu hasa baada ya kupata ushindi wa magoli mawili kwa moja katika mechi yao ya mwanzo dhidi ya Japan.

Rodriguez ambaye amelijaza pengo la mshambuliaji mwenzake ambaye alikosa tamasha hilo kupitia jeraha, Radamel Falcao amesema ulikuwa mchuano mgumu kamatu ilivyo michuano yote ya Kombe la Dunia.

Fifa WM 2014 Elfenbeinküste Kolumbien
Gervinho alionyesha umahiri wake kwa kuifungia Cote d'Ivoire goli la juhudi za kibinafsiPicha: Pedro Ugarte/AFP/Getty Images

Ameongeza kuwa ni furaha kwao kupata pointi mbili kutoka kwa mpinzani wao ambaye ana nguvu nyingi na anayefahamu kucheza kandanda safi. Kocha wa Colombia Jose Pekerman amesema amefurahishwa na mahala walikofikia, wakati wakilenga kufuzu katika duru ya pili kwa mara ya pili pekee katika Kombe la Dunia ambalo wamecheza mara tano.

Mwenzake wa Cote d'Ivoire Sabri Lamouchi alionekana kutokubaliana na matokeo hayo. Alisema hawakustahili kuupoteza mchuano huo. Mchezaji huyo wa zamani wa Ufaransa amesema Colombia ina wachezaji wenye ujuzi mwingi na waliwasubiri kufanya makosa kabla ya kuwaadhibu.

Serey Die abubujikwa machozi

Wakati wa kuchezwa nyimbo za taifa, kiungo wa Cote d'Ivoire Serey Die alibubujikwa machozi --- ambapo baadaye iliripotiwa kuwa alikuwa amefiwa na babake saa chache tu kabla ya kuanza mchuano huo. Vijana hao wa Afrika walimwacha Didier Drogba kwenye benchi la akiba, kabla ya kumwingiza uwanjani baada ya kipindi cha pili.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo