1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Comey amlaumu Trump kwa kusema uongo

Mohammed Khelef
8 Juni 2017

Mkuu wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Marekani (FBI) James Comey, amehojiwa na Kamati ya Ujasusi ya Bunge juu ya jukumu la Rais Donald Trump katika uchunguzi wa uingiliaji kati wa Urusi katika uchaguzi.

https://p.dw.com/p/2eLo6
USA Anhörung James Comey, früherer FBI-Direktor
Picha: Getty Images/AFP/C. Somodevilla

Licha ya kutoonesha moja kwa moja kwamba Urusi ilishiriki kwenye udukuzi wa mfumo wa uchaguzi wa Marekani, Comey ameeleza kuwa FBI ilifahamu juu ya udukuzi huo kwenye majira ya kiangazi ya mwaka 2015, na pia kukanusha kuwa alitakiwa na Trump kuachana na uchunguzi wa suala hilo. 

Hata hivyo, kwa kauli ya wazi kabisa, Comey ameulaumu utawala wa Rais Trump kwa kile alichosema kutumia uongo katika kuzungumzia namna yeye mwenyewe alivyoondolewa kwenye nafasi yake ya ukuu wa FBI, licha ya awali kuelezwa na mwenyewe Trump jinsi alivyo na uweledi kwenye kazi yake.

"Ingawa sheria haihitaji pawepo na sababu yoyote katika kumfuta kazi mkurugenzi wa FBI, utawala wa Trump ulichaguwa kunifedhesha mimi na zaidi FBI nzima kwa kusema kuwa shirika hili liko kwenye mkanganyiko, kwamba linaongozwa vibaya, na kwamba wafanyakazi wamepoteza imani na kiongozi wake. Huo ulikuwa ni uongo dhahiri shahiri," alisema Comey.

Taarifa kutoka ndani ya Kamati ya Ujasusi ya bunge la Marekani zinasema kuwa ushuhuda wa kimaandishi wa Comey unaonesha kuwa Rais Trump alimtishia mkurugenzi huyo kuhusu kazi yake na kumtaka aache kuendelea na uchunguzi dhidi ya mshauri wake mkuu, Michael Flynn, jambo ambalo linakwenda kinyume na muongozo unaozuwia uingiliaji wa kisiasa kwenye upelelezi wa FBI.

Ushahidi wa kukera na kuudhi

USA Anhörung James Comey, früherer FBI-Direktor
Kikao cha Kamati ya Ujasusi ya Bunge la Marekani kikiendelea kumuhoji James Comey, mkurugenzi wa zamani wa FBI, juu ya dhima ya Rais Donald Trump kwenye uchunguzi juu ya uingiliaji kati wa Urusi katika uchaguzi wa 2016.Picha: Reuters/J. Bourg

Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo kutokea chama cha Democrat, Mark Warner, alisema kuwa ushuhuda uliowasilishwa na Comey leo unakera na kuudhi, ingawa uchunguzi unaofanyika sasa hauhusiani na siasa za uchaguzi mwa mwaka jana, ambao umemuingiza madarakani Rais Trumpm, bali misingi ya taifa la Marekani.

"Kwa ukweli uchunguzi huu hauhusiani na kuutia dosari uchaguzi uliopita. Sio kuhusu nani alishinda, nani alipoteza, sio kuhusu Republicans na Democrats. Tupo hapa kwa kuwa mamluki wa kigeni walitushambulia nyumbani petu, sio kwa bunduki wala mizinga, bali kwa kupanga njama dhidi ya mchakato wetu wa kidemokrasia, uchaguzi wetu." Alisema Warner.

Mapema akimkaribisha Comey kutoa ushuhuda wake, mwenyekiti wa kamati ya Ujasusi kutoka chama cha Republican, Richard Burr, alimtaka Comey kusema kila kitu ambacho kilitokea kwenye mkasa huo, akimuhimiza kuwa kauli yake ina maana kubwa kwa watu wa Marekani.

"Wakati tukiliangalia kwa undani suala la uwezekano wa kuingiliwa kati na Urusi kwenye uchaguzi wa 2016, waraka wako umetaja mazingira na uhalisia wa mazungumzo yako na Rais Trump, na hivyo Wamarekani sasa wanataka kujuwa kutoka kwako mwenyewe kama ambavyo watataka kumsikia Rais naye kwa upande wake," alisema Burr.

Tayari taarifa za ndani kutoka Ikulu ya Marekani zilishagusia kuwa Trump anakanusha kumtaka Comey kuachana na uchunguzi huo, shitaka kubwa kabisa ambalo kama likithibiti linaweza kumfanya aondolewe madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani. 

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf