1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Condoleezza Rice atetea misaada ya kijeshi

P.Martin1 Agosti 2007

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani,Condoleezza Rice alie zirani katika Mashariki ya Kati ametetea mpango wa kuzipa nchi za kanda hiyo misaada ya kijeshi,kama ilivyopendekezwa na Rais Bush hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/CHAD
Waziri wa nje Rice(katikati) na Waziri wa ulinzi Gates(kushoto) wakikutana na Rais Hosni Mubarak wa Misri(kulia) katika mji wa pwani Sharm-el-Sheikh nchini Misri
Waziri wa nje Rice(katikati) na Waziri wa ulinzi Gates(kushoto) wakikutana na Rais Hosni Mubarak wa Misri(kulia) katika mji wa pwani Sharm-el-Sheikh nchini MisriPicha: AP

Mchakato wa amani katika Mashariki ya Kati na mpango unaohusika na misaada ya kijeshi ya mabilioni kadhaa,ni mada zilizopewa kipaumbele katika majadiliano ya waziri wa nje wa Marekani Bibi Condoleezza Rice pamoja na mawaziri wenzake wanane kutoka Umoja wa Nchi za Kiarabu,mjini Sharm el-Sheikh.Wote walikubaliana kuwa katika kutafuta suluhisho la amani,matatizo ya kanda hiyo yasitenganishwe bali yapaswa kutazamwa kwa umoja na kupatiwa suluhisho kwa pamoja.

Waziri Rice aliefuatana na waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates katika ziara yake ya Mashariki ya Kati,aliuambia mkutano wa waandishi wa habari katika mji wa mapumziko wa Sharm el-Sheikh nchini Misri,azma ya mpango huo wa kijeshi ni kuwasaidia washirika wa Marekani katika Mashariki ya Kati,kupiga vita ugaidi.Akasisitiza kuwa kuna mchakato wa utendaji na diplomasia nzito pia.Akaongezea kuwa mchakato huo wa kidiplomasia utafungamana na juhudi za kuwasaidia washirika wa Marekani kujihami dhidi ya vitisho.

Hata mkutano wa amani uliopendekezwa na Rais George W.Bush kati kati ya mwezi Julai ulijadiliwa.Wajumbe wote walikubaliana kuwa kabla ya hapo lakini,kuna haja ya kuwa na mazungumzo ya kidiplomasia na kufanya matayarisho ya mkutano huo.Lakini tarehe ya mkutano huo wa amani haikupangwa.

Wakati huo huo,waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia,Mwanamfalme Saud al-Faisal alipozungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari pamoja na Rice na Gates mjini Jeddah,aliarifu kuwa nchi yake inauunga mkono mkutano uliopendekezwa na Bush.Akasema,Saudia itakapopokea mwaliko kutoka waziri wa nje wa Marekani,itauzingatia mwaliko huo kwa dhati na itapendelea kushiriki katika mkutano huo.Akashauri kuwa mkutano huo ujadili masuala ya kimsingi ili kuweza kupata amani katika Mashariki ya Kati.Akaongezea kuwa Israel nayo ichukuwe hatua ya kuelekea kwenye amani.

Kwa upande mwingine,taarifa iliyotolewa asubuhi ya leo na ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Ehud Olmert imesema,ni matumaini yake kuwa nchi nyingi za Kiarabu,ikiwa ni pamoja na Saudi Arabia, zitahudhuria mkutano huo wa kimataifa.Wakati huo huo maafisa wa Kiisraeli waliozungumza kwa sharti kuwa wasitajwe majina wamesema,ni matumaini yao kuwa mkutano huo wa kimataifa utaleta maendeleo ya kidiplomasia kati ya Israel na Saudi Arabia.Nchi hizo mbili hazina uhusiano wa kibalozi.

Waziri Rice akielekea Jerusalem,baadae hii leo anatazamia kuwa na majadiliano pamoja na maafisa wa Kiisraeli na Kipalestina kwa azma ya kupiga jeki juhudi za amani.