1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Condoleezza Rice Mashariki ya Kati tena

Kalyango Siraj6 Novemba 2008

Waziri wa mashauri ya Kigeni wa Marekani Condoleezza Rice ameanza safari nyingine ya mashariki ya kati yenye nia ya kufufua mazungumzo ya kuleta amani kati ya Palestina na Israel.

https://p.dw.com/p/FoRr
Condoleezza RicePicha: AP

Hata hivyo ziara yake imekuja wakati ghasia zikianza tena kati ya Israel na ukanda wa Gaza ambapo inaarifiwa kuwa takriban wapalestina sita wameuawa na majeshi ya Israel.

Israel imesema alhamisi kuwa inapendelea kurefusha makubaliano ya kusitisha mashambulio ndani na nje ya eneo la Gaza,licha ya kutokea kwa ghasia zilizopelekea waPalestina saba kuuawa na kufuatiwa na uvurumishaji wa maroketi kadhaa ndani mwa taifa la kiyahudi.

Naibu waziri wa Ulinzi wa Israel, Matan Vilnai, ameiambia Redio ya jeshi la Israel kuwa, anatumai kuwa makubaliano hayo yataweza kuendelea tena kwani wanayaamini na mambo yanaonekana kama yanatulia.

Matamshi yake yamekuja siku moja baada ya wanaharakati wa Kipalestina kutoka ukanda wa Gaza kuvurumisha maroketi ndani mwa Israel ingawa inasemekana hayakusababisha majeruhi yoyote. Uvurumishaji huo unatokana na hatua ya operesheni ya kijeshi iliofanywa na vikosi vya usalama vya Israel ndani mwa eneo linalozingirwa na kupelekea kuwauwa wapiganaji saba wa kipalestina.

Vilnai amesema kuwa vikosi vya Israel vilitumwa Gaza Jumanne usiku ili kulipua handaki ambazo zilikuwa zitumiwe na wanaharakati kwa shughuli za kuishambulia Israel na hivyo kuvuruga makubaliano ya kutoshambuliana.

Makubaliano hayo yamekuwa yanaheshimiwa na pande zote kwa kipindi cha miezi minee. Makubaliano hayo ya lifikiwa kwa ushiriano na Misri na visa vya jumanne na jumatano ndio vibaya kuwahi kutokea tangu yaanze kutekelezwa Juni 19.

Aidha yametokea wakati waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice,akifunga safari kuelekea eneo la mashariki ya kati kwa lengo la kuyapiga jeki mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina na kuona kama anaweza akazishawishi pande husika kuafikiana kuweka tarehe ya kukubaliana kupatikana amani ya kudumu kabla ya mwaka huu kumalizika kama ulivyo ahidi utawala wa Bush.

Hata hivyo zimesalia siku 77 utawala wa Bush uondoke ofisini na haijulikani ikiwa lengo lake la kupatikana kwa mkataba wa amani mashariki ya kati litafikiwa. Ndoto hiyo inakabiliwa na vizingiti kadhaa kama vile,kila upande baado unashuku mwingine na pia visa vya siku mbili zilizopita katika ukanda wa Gaza vinaeleza utete wa hali hiyo.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, katika safari yake ya nane mashariki ya kati, pia anatarajiwa kufika Misri na Jordan,inafikiriwa ili kuomba msaada wa waarabu kuhusiana na mazungumzo ya amani.

Taarifa zaidi zaonyesha kama mkutano wa wapatanishi wa mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati utafanyika mwishoni mwa juma nchini Misri. Utahudhuriwa,miongoni mwa wengine, na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas,waziri wa mashauri ya kigeni wa Israel Tzipi Livni pamoja na waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice.

Rais mteule wa Marekani, Barack Obama, amesema kuwa moja wa mikakati ya utawala wake ni kutanzua mgogoro kati ya Palestina na Israel.