1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Conte awaonya wachezaji wake kutobweteka

Bruce Amani
1 Mei 2017

Kinyang'anyiro cha ubingwa wa Ligi ya Premier ya England kimepamba moto, ambapo vinara Chelsea wanaongoza na pengo la pointi nne tu dhidi ya nambari mbili Tottenham Hotspurs

https://p.dw.com/p/2cC6l
UK | Fußball | Crystal Palace vs Chelsea - Premier League -  Selhurst Park Stadium
Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS/D. Klein

Kocha  wa  viongozi  wa  ligi hiyo Antonio Conte  amewaonya  wachezaji  wake kutobweteka  na  ushindi  wa  mabao 3-0  dhidi  ya  Everton na  kufikiri  kwamba  ubingwa  ni  wao  tu. Kikosi  cha Conte  kimejiimarisha   katika  nafasi  yake  juu  kileleni mwa  msimamo  wa  ligi, Jumapili, lakini timu  iliyoko katika  nafasi  ya  pili  Tottenham inawafuatia  nyuma  kwa kasi  ya  ajabu.

Lakini  wakati  vijana  hao  wa  Conte  wakirejea  nyumbani na  ushindi  huo , Tottenham  walikuwa  wanapata  ushindi wao  muhimu dhidi  ya  Arsenal na  kujiweka  katika  nafasi ya  kuitikisa  Chelsea  katika  nafasi  ya  kwanza.

Hata  hivyo kocha  wa  Arsenal, Aserne  Wenger  amesema hatasalim  amri  kuingia  katika  eneo  la  timu  nne bora  za juu  katika  Premier League  msimu  huu  licha  ya  kipigo hicho  cha  mabao 2-0  dhidi  ya  Tottenham  Hotspurs , hali  inayoashiria  kwamba  Arsenal  mara  hii  itamaliza chini  ya  mahasimu  wao  hao kwa  mara  ya  kwanza katika  miaka  21  kocha  huyo  akiwa  katika  klabu  hiyo.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri: Iddi Ssessanga