1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CORD walalamikia matokeo Kenya

6 Machi 2013

Viongozi wa muungano CORD wamelalamikia namna matokeo ya kura yanavyotolewa, huku waangalizi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na wa Soko la Pamoja la COMESA wakitoa ripoti zao za awali.

https://p.dw.com/p/17rFD
Kenyan Prime Minister Raila Odinga (L), Vice President Kalonzo Musyoka (C) and Trade Minister Moses Wetangula gesture at supporters in Nairobi on December 4, 2012 after agreeing to form a powerful alliance as running mates in presidential elections due in March 2013. The former rivals along with leaders of 10 other smaller parties, signed an agreement in front of thousands of supporters to form the Coalition for Reform and Democracy (CORD) party. Odinga is widely tipped to be the presidential candidate with Musyoka as his deputy, although no formal announcement was made. AFP PHOTO / TONY KARUMBA (Photo credit should read TONY KARUMBA/AFP/Getty Images)
Kenia Wahlen Raila OdingaPicha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Huku matokeo ya uchaguzi yakizidi kutiririka kutoka katika kituo cha kuhesabia kura jijini Nairobi, viongozi wa muungano wa CORD wamelalamika kwamba utaratibu unaotumiwa kutangaza matokeo hayo unatia shaka.

Kulingana na taarifa iliyosomwa na Kalonzo Musyoka, mgombea mwenza wa Raila Odinga, viongozi kutoka vyama vinavyounda muungano huo wameowaomba wafuasi wao kuwa watulivu wakati matokeo yote yanavyosubiriwa.

Kalonzo alisema kuwa bado wana uhakika wa kushinda katika uchaguzi na akaongeza kuwa endapo watashindwa wako tayari kusalimu amri.

Kauli ya CORD yanakuja wakati ambapo kinara wa mrengo wa Jubilee, Uhuru Kenyatta, anaonekana kuongoza katika matokeo ya awali yaliyotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Hata hivyo, Kenyatta na mpinzani wake wa karibu Odinga wanamenyana vilivyo huku kila mmoja wao akiwa ametimiza zaidi ya kura milioni mbili.

Katika mkutano na waandishi wa habari, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Bw. Isaack Hassan amewaomba wanasiasa wawe watulivu wakati huu wa kuhesabiwa kwa kura na akakiri kuwa kulikuwa na hitilafu Fulani za kimitambo ambazo zilichangia kucheleweshwa kwa matokeo.

Hata hivyo, mgombea mwenza wa muungano wa Jubilee, William Ruto, alisiifu IEBC kwa kuendeleza shughuli za uchaguzi kwa utaratibu unaofaa. Ruto amewashukuru Wakenya kwa kujitokeza kwa wingi ili kupiga kura siku ya Jumatatu.

COMESA, EAC watoa ripoti ya awali

Wakati huo huo, tume ya wangalizi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na mataifa wanachama wa COMESA imetoa ripoti yao ya mwanzo kuhusiana na zoezi nzima la uchaguzi.

Wafuasi wa muungano wa CORD.
Wafuasi wa muungano wa CORD.Picha: Ivan Lieman/AFP/Getty Images

Kiongozi wa ujumbe huo, Abdulrahman Kinana kutoka Tanzania, amesema kuwa uchaguzi wa Kenya uliendeshwa kwa njia ya kidemokrasia na kuisifu tume ya uchaguzi kwa kutekeleza wajibu muhimu kulingana na katiba.

Hadi kufikia majira ya jioni, kura bado zilikuwa zikihesabiwa na matokeo kamili yanatarajiwa wakati wowote. Kwa mujibu wa katiba, tume inayo nafasi ya kutoa matokeo yote katika kipindi cha wiki nzima tokea siku ya kupiga kura.

Mwandishi: Reuben Kyama/DW Nairobi

Mhariri: Mohammed Khelef