1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CORD wataka zoezi la kuhisabu kura lisimamishwe

7 Machi 2013

Muungano cha CORD nchini Kenya umetaka zoezi la kuhisabu kura za uraisi nchini humo lsitishwe na kuelezea wasiwasi wake juu ya uadilifu wa zoezi ambalo siku tatu baada ya upigaji kura limeshindwa kukamilika.

https://p.dw.com/p/17sga
Kalonzo Musyoka, the running mate of Kenya's presidential candidate Raila Odinga, speaks during a news conference in Nairobi March 7, 2013. Musyoka called for the vote count to be halted on Thursday and cast doubt on the fairness of a process that is still incomplete three days after the poll, remarks that could inflame a largely peaceful election. REUTERS/Siegfried Modola (KENYA - Tags: ELECTIONS POLITICS)
Kenia Musyoka PK Stimmenauszählung AnhaltenPicha: Reuters

Kauli hii inatajwa kwamba inaweza kuutia kasoro kubwa uchaguzi wa hapo Jumatatu (tarehe 4 Machi), ambao hadi sasa umetajwa na waangalizi wa kimataifa kwamba ulikuwa wa amani na wa wazi.

Mgombea wa CORD, Waziri Mkuu Raila Odinga, yuko nyuma ya mgombea wa muungano wa Jubilee, Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta, wakati kura zikiendelea kuhesabiwa.

Hata hivyo, mgombea mwenza wa Odinga, Kalonzo Musyoka (pichani juu), amesema kauli ya muungano huo haipasi kuchukuliwa kama wito wa umma kuchukua hatua na amewataka wapiga kura kuendelea kuwa watulivu na wastahmilivu.

Ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 nchini humo, zilipelekea kiasi cha watu 1,200 kuuawa na zaidi ya 600,000 kulazimika kuyahama makaazi yao.

"Sisi kama muungano wa CORD tunaamini kwamba zoezi hili la kuhisabu kura limekosa uhalali na lazima lisimamishwe na liazishwe upya kwa kutumia fomu kutoka vituo vya kupiga kura," Musyoka aliwaambia waandishi wa habari.

"Tuna ushahidi kwamba matokeo tunayopokea 'yamechezewa,'" alisema.

Tume kuendelea kuhisabu kura

Hata hivyo, afisa mmoja wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ameliambia Shirika la Habari la Reuters kwamba zoezi la kuhisabu kura halitasitishwa.

Viongozi wa muungano wa CORD, Raila Odinga (kushoto), Kalonzo Musyoka (katikati) na Moses Mutangula.
Viongozi wa muungano wa CORD, Raila Odinga (kushoto), Kalonzo Musyoka (katikati) na Moses Mutangula.Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Tume hiyo imekuwa ikisisitita kwamba zoezi zima limekwenda kwa haki na uwazi na kwamba matokeo ya uchaguzi huo hayataathiriwa na kuharibika kwa mitambo ya kieletroniki ya kuhesabia kura, ambayo imelifanya zoezi hilo kwenda taratibu.

Kufikia sasa, Kenyatta anayekabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kikabila katika Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) anaongoza katika matokeo hayo, huku karibuni nusu ya kura zikiwa zimeshahisabiwa.

Wafadhili kutoka nchi za Magharibi, wanaotoa msaada wa mamilioni ya dola nchini Kenya kila mwaka, tayari wameonyesha kuwa kushinda kwa Kenyatta kutaathiri uhusiano wa kidiplomasia.

Idadi ya kura zilizoharibika

Mwenyekiti wa IEBC, Ahmed Issack Hassan, amesema kuhisabiwa kwa kura huenda kukakamilika siku ya Ijumaa au Jumatatu, ambayo ni siku ya mwisho kwa mujibu wa sheria, ambapo matokeo hayo yanapaswa kutangazwa.

Mwenyekiti wa IECB, Ahmed Issack Hassan (kushoto).
Mwenyekiti wa IECB, Ahmed Issack Hassan (kushoto).Picha: James Shimanyula

Pamoja na kufeli kwa mfumo wa kieletroniki wa kuhisabia kura, jambo jengine linaloweza kuzua mzozo ni iwapo idadi kubwa ya kura zilizokataliwa itahesabiwa katika matokeo ya jumla, maana hatua hiyo inaweza kumzuia Kenyatta kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura ambazo mgombea urais anapaswa kupata ili ashinde katika duru ya kwanza. Kwa sasa tume ya uchaguzi inatangaza idadi ndogo ya kura zilizokataliwa ukilinganisha na hapo awali.

“Nataka pia kusisitiza kuwa licha ya kuacha kutumia mfumo wa kuhesabu kura wa elekroniki, haimaanishi kuwa uadilifu wa matokeo umeharibika,” Mwenyekiti wa IEBC, Issack Hassan, amewaambia waandishi wa habari.

Wakenya wengi wanasema wameamua hawatakubali uchaguzi kusababisha mzozo wa kikabila, baada ya uchaguzi uliopita kuathiri nchi hiyo yenye uchumi mkubwa Afrika ya Mashariki.

Mwandishi: Dalila Athman/Mohammed Khelef/Reuters/dpa
Mhariri: Saumu Mwasimba