1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CR7 arejea kwa kishindo

27 Desemba 2014

Mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo hajaridhika na mataji manne aliyoshinda 2014 ikiwa ni pamoja na Kombe la pili la Ligi ya Mabingwa Ulaya, na analenga kuimarika hata zaidi katika mwaka ujao

https://p.dw.com/p/1EAbo
FC Barcelona vs. Real Madrid 25.10.2014
Picha: AFP/Getty Images

CR7 alifunga mabao 51 katika mechi 41 za msimu uliopita, na kuweka rekodi ya magoli 17 katika ligi ya mabingwa Ulaya, wakati Real Madrid wakiirefusha rekodi yao kwa kushinda Kombe la 10 la Ulaya na Kombe la Mfalme.

Na nyota huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 29, ameendelea alikoachia msimu uliopita katika msimu wa 2014-15, wakati klabu hiyo tajiri zaidi ulimwenguni katika mapato, ikinyakua taji la European Super Cup na klabu bora ya kandada Ulimwenguni yaani Club World Cup, na amejikusanyia magoli 32 katika mechi 25 katika michezo yote.

Kombobild
Neuer, Messi na Ronaldo wanawania tuzo ya Ballon d'OrPicha: Getty Images/Reuters

Magoli yake 25 katika mechi 14 za ligi ya Uhispania ni rekodi mpya nchini humo na anaonekana kuivunja rekodi ya idadi kubwa zaidi ya magoli kuwahi kufungwa katika msimu mmoja wa La Liga, ya mabao 50 yaliyofungwa na Lionel Messi katika msimu wa 2011-12

CR7 ameliambia gazeti la Uhispania la AS kuwa itakuwa kama ndoto kwake kama mwaka wa 2015 utakuwa kama 2014 au hata bora zaidi. Anasema hilo linawezekana kwa sababu Madrid ni timu inayotaka kuhusika katika mashindano yote.

Ronaldo atajua kama atashinda kwa mara ya tatu Tuzo ya FIFA ya Mchezaji Bora wa Mwaka, maarufu kama Ballon d'Or na yake ya pili mfululizo, mnamo Januari 12 wakati atakaposhindana na nahodha wa Argentina Lionel Messi anayechezea Barcelona na mlinda lango wa Ujerumani na Bayern Munich Manuel Neuer.

Na wakati CR7 akipigiwa upatu kushinda tuzo hiyo, mshindi wa Kombe la Dunia kipa Manuel Neuer amesema itakuwa vigumu kwake kuwapiku Ronaldo na Messi katika kushinda tuzo hiyo.

Neuer ameliambia gazeti la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung kuwa Ronaldo na Messi ni nguli wa kimataifa na hiyo wana faida kumliko. Kama Neuer atashinda Ballon d'Or, atakuwa Mjerumani wa kwanza kufanya hivyo tangu Lothar Matthaus aliposhinda 1990 na mlinda lango wa pili pekee kuwahi kushinda baada ya Lev Yashin, aliyekuwa wakati huo wa Muungano wa Kisovieti mwaka wa 1963.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters/dpa
Mhariri: Mohammed Dahman