1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CR7 ashinda Ballon d'Or 2014

13 Januari 2015

Cristiano Ronaldo aliwapiku Manuel Neuer na Lionel Messi na kushinda tuzo ya Ballon d'Or, lakini kocha wa timu ya taufa Joachim Löw na kiungo wa Wolfsburg Nadine Kessler walikuwa washindi wa Ujerumani

https://p.dw.com/p/1EJME
FIFA Ballon d'Or Gala Cristiano Ronaldo Weltfußballer 2014 12.01.15
Picha: Reuters//Ruben Sprich

Cristiano Ronaldo alishinda tuzo yake ya tatu ya mchezaji bora wa mwaka ulimwenguni - FIFA Ballon d'Or 2014 na kumshinda mlinda lango wa Ujerumani Manuel Neuer na Muargentina Lionel Messi.

Neuer aliibuka katika nafasi ya tatu nyuma ya mshindi mara nne wa tuzo hiyo Lionel Messi katika kura zilizopigwa na manahodha na makocha wa timu za taifa kutoka nchi 209 wanachama wa FIFA, pamoja na waandishi habari kadhaa walioteuliwa.

Joachim Löw FIFA Ballon d'Or Welttrainer 2014 12.01.15
Joachim Löw kocha bora wa mwaka wa 2014Picha: Olivier Morin/AFP/Getty Images

Ujerumani hata hivyo haikuondoka Zurich bila ya tuzo yoyote. Katika kitengo cha wanawake, Kiungo wa Wolfsburg Mjerumani Nadine Kessler aliwapoku Marta wa Brazil na Mshambuliaji wa Marekani Abby Wambach kwa kunyakuwa tuzo ya mchezaji bora mwanamke ulimwenguni. Kocha wa Wolfsburg Ralf Kellermann alichaguliwa kuwa kocha bora wa kandanda la wanawake.

Kellermann aliiongoza timu ya Wolfsburg akiwemo Kessler kushinda mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili mfululizo.

Kocha wa timu ya Ujerumani Joachim Löw alishinda tuzo ya kocha bora wa mwaka, mbele ya Carlo Ancelloti wa Real Madrid na Diego Simeone wa Atletico Madrid.

James Rodriguez alishinda tuzo ya Puskas ya goli bora la mwaka, kutokana na kombora alilofyatua langoni wakati akiichezea Colombia dhidi ya Uruguay katika Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.

Timu ya bora ya mwaka ya FIFA ni kama ifuatavyo: Manuel Neuer (Ujerumani, Bayern Munich) - Sergio Ramos (Uhispania, Real Madrid), Thiago Silva (Brazil, PSG), David Luiz (Brazil, PSG), Philipp Lahm (Ujerumani, Bayern Munich) - Andres Iniesta (Uhispania, Barcelona), Toni Kroos (Ujerumani, Real Madrid), Angel Di Maria (Argentina, Manchester United) - Arjen Robben (Uholanzi, Bayern Munich), Lionel Messi (Argentina, Barcelona), Cristiano Ronaldo (Ureno, Real Madrid)

Mwandishi. Bruce Amani
Mhariri. Sekione Kitojo