1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cristiano Ronado

12 Januari 2009

Je, atatawazwa leo zurich "mwanasoka wa mwaka wa FIFA ?

https://p.dw.com/p/GWa6
Cristiano Ronaldo. +++Picha: picture-alliance/ dpa

Cristiano Ronaldo -jogoo la Manchester United na Ureno, latazamiwa kuchaguliwa leo "mwanasoka bora wa mwaka wa FIFA" mjini Zurich-

Manchester United yatamba mbele ya Chelsea katika Premier League.Harambee Stars (Kenya) yaipiga kumbo Taifa Stars (Tanzania) katika nusu-finali ya Kombe la CECAFA mjini Kampala na kombe la vijana la Afrika laanza huko Ruanda mwishoni mwa wiki ijayo.

kinyanganyiro cha kombe la Challenge Cup -kanda ya Afrika Mashariki na kati kimefikia kilele chake baada ya jana Kenya kuilaza Tanzania mjini Kampala mabao 2-1 na wenyeji Uganda kuitimua burundi kwa mabao 5-0 mjini kampala. Wenyeji Uganda wana miadi kesho na Harambee Stars Kenya kwa finali ya mwaka huu ya kombe hilo la CECAFA-kombe la kanda ya Afrika mashariki na kati.

Kombe la vijana la Afrika likitazamiwa kuanza nchini Ruanda mwishoni mwa wiki ijayo, huko Zurich, makao makuu ya FIFA ,anatawazwa leo usiku"mwanasoka bora wa mwaka wa FIFA".

Wingi wa ureno na Manchester United Christiano Ronaldo anapigiwa upatu kuwa ndie atakaevaa taji hilo leo usiku katika hafla maalumu itakayofanyika Jumba la Opera la Zurich.

Christiano Ronaldo anakwenda katika hafla hiyo jioni hii huko Zurich akiwa tayari ni bingwa wa Ulaya,Dunia na wa Uingereza -Premier League.Isitoshe,ameshachaguliwa "mchezaji bora kabisa wa dimba wa mwaka wa Ulaya"-European footballer of the year.

Matumaini kwa Christiano Ronaldo kuvaa taji hili leo ni makubwa kwa sababu wenzake waliovaa kwanza taji la ulaya kama vile Ronaldinho, Kaka wa Brazil, Fabio Cannavaro wa Itali, baadae walichaguliwa pia wanadimba wa mwaka wa FIFA.

Stadi wa Brazil na AC Milan, Kaka kwa mara nyengine tena yumo katika orodha fupi ya mastadi 5 watakaopigiwa kura leo. Wengine ni Lionel Messi wa FC Barcelona kutoka Argentina na stadi wa Spain na FC Liverpool Fernando Torres,alietia lile bao la ushindi lilililoitawaza Spain mwaka jana mabingwa wa Ulaya.

Messi alishinda medali ya dhahabu ya olimpik kwa Argentina wakati kaka mwaka jana alitoka mikono mitupu.

Mfaransa Zinedine Zedane ni mchezaji pekee wa dimba wa dunia kutoka timu bingwa ya dunia hapo mwaka 2000 na hii tangu taji hilo kuanzishwa 1991.

Mafanikio ya kutawazwa kwa Manchester United mabingwa wa dunia, Ulaya na wa Uingereza na Ronaldo akiwa usoni mwa ushindi wa timu hiyo, kunampa nafuu ya kushinda leo kuliko wenzake.

Ronaldo aliligonga gari lake la "Ferrari" na kulibomoa,lakini kwa mabao yake 42 aliotia msimu uliopita na kuiwezesha Man U kutwaa ubingwa wa ulaya na dunia, yanatosha kumvika taji leo usiku.

Ikiwa Ronaldo wa Manchester United au Torres wa Liverpool, mmoja wao atashinda taji hilo leo, basi huo utakuwa ushindi mkuu wa Premier League katika dimba la dunia.

Hadi sasa wachezaji wote bora wa dimba wa dunia kuanzia Lothar Matthaeus wa Ujerumani lilipoanzishwa taji hili 1991 hadi Kaka wa Brazil mwaka 2007 wametokana ama na Ligi za Itali au Spain.

Upande wa dimba la akina dada,stadi na mchawi wa Brazil, Marta,

anaania nae leo usiku taji lake la 3 la dunia .Wapinzani wake ni mbrazil mwenzake Cristiane,muingereza Kelly Smith na mjerumani Nadine Angerer na mwenzake Birgit Prinz.Birgit Prinz alivaa taji hilo la mwanasoka bora wa kike wa dunia mara 3 mfululizo-kuanzia 2003-2005.

Ama katika Ligi mashuhuri barani Ulaya,Manchester United ilitamba tena jana mbele ya mahasimu wao Chelsea huko Old Trafford walipowachezesha kindumbwendumbwe na kuwazaba mabao 3-0.Kwa ushindi huo na kwa uzembe wa Liverpool kileleni,Manchester United sasa inanyatia taji la Premier League kutoka nafasi ya 3 nyuma ya Chelsea kwa pointi 1 tu.Vidic,Rooney na Berbatov walipiga misumari hiyo 3 katika jeneza la Chelsea.Laiti chelsea ingelishinda jana ingejikuta iko pointi 1 tu nyuma ya viongozi wa Ligi FC Liverpool. Liverpool imeshindwa kutumia nafasi yake na kupanua mwanya hadi pointi 6 lakini walizimwa na Stoke City hapo jumamosi kwa kutoka sare 0:0.

Katika la Liga, Ligi ya Spain, Real Madrid imesogea mbele hadi nafasi ya pili ya ngazi ya ligi kati yake na Sevilla baada ya kutandika Mallorca mabao 3-0.Sevilla ilishinda Deportivo la Coruna kwa mabao 3-1. Real na sevilla ziliopo nafasi ya pili,hata hivyo, zipo pointi 9 nyuma ya viongozi wa Ligi FC Barcelona. Lionel Messi kutoka Argentina, aliipa Barcelona ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Osasuna.

Mkwaju wa (freekick ) aliouchapa Del Piero katika changamoto za Serie A-Ligi ya Itali , ulitosha kuinyanyua Juventus juu na kuipatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Siena. Sasa Juventus iko nyuma kwa pointi 4 kutoka walipo viongozi wa ligi Inter Milan.