1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Croatia yaionjesha Uhispania kichapo

22 Juni 2016

Timu sita zimetinga katika hatua ya mchujo ya michuano ya ubingwa wa Ulaya. Ni timu moja pekee, Jamhuri ya Czech, iliyofungishwa virago katika dimba hilo. Uturuki na Albania zilibaki na matumaini lakini sio ya hakika

https://p.dw.com/p/1JAyt
Frankreich Fußball-EM Spanien vs. Kroatien
Picha: Reuters/M. Dalder

Timu nane zitakazoshuka dimbani leo zinafahamu kile zinapaswa kufanya hasa ili kubakia nchini Ufaransa.

Lakini kuna mtanange mmoja mkali unaosubiriwa katika dimba la Euro 2016 ambalo limeanza kupamba moto. Mabingwa watetezi mara mbili Uhispania wataangushana na Italia Jumatatu ijayo katika uwanja wa Stade de France wenye uwezo wa kuwa na mashabiki 75,000. Itakuwa ni marudio ya fainali ya Euro 2012. Uhispania ilijikuta katika mchuano huo usiohitajika dhidi ya adui wake wa zamani baada ya kufungwa bao katika dakika ya 87 katika kichapo cha 2-1 dhidi ya Croatia jana usiku.

Ushindi huo una maana Croatia iliongoza Kundi D na imezawadiwa mchuano dhidi ya moja ya timu zitakazomaliza katika nafasi ya tatu kwenye makundi. Hilo litajulikana wazi wakati duru ya mwisho ya michuano ya makundi itachezwa leo.

Frankreich Fußball-EM Deutschland vs. Nordirland Mario Gomez Jubel
Mario Gomez aliifungia Ujerumani bao safiPicha: Reuters/J. Sibley

Awali, Croatia ilikuwa moja ya timu tano ambazo nafasi yao katika hatua za mchujo ilihakikishwa kutokana na ushindi wa Ujerumani na Poland wa bao moja kwa bila kila mmoja katika Kundi C, dhidi ya Ireland ya Kaskazini na Ukraine ambayo tayari imeyaaga mashindano.

Ujerumani ilifuzu kama mshindi wa kundi lake na Poland kama nambari mbili. Lakini matokeo hayo pia yalikiweka kiwango cha pointi nne kuwa hakikisho la kubakia Ufaransa kwa angalau mchuano mmoja zaidi.

Croatia, Hungary na Slovakia tayari zilikuwa zimefikia kiwango hicho na hivyo zikafuzu. Mfumo mpya wa Euro 2016 ambapo kuna timu 24 una maana kuwa nne kati ya timu sita zitakazomaliza katika nafasi ya tatu zitafuzu ili kujumuisha kundi la timu 16 za mwisho, pamoja na timu mbili za kwanza katika kila kikundi.

Kichapo cha Ireland ya Kaskazini dhidi ya Ujerumani mwishowe hakikuwa kibaya maana timu hiyo ilithibitishwa baadaye kuwa moja ya timu za nafasi ya tatu zilizofuzu. Hiyo ni kutokana na matokeo ya mchuano mwingine wa kundi la Uhispania na Croatia ambapo Uturuki iliifunga Jamhuri ya Czech 2-0.

Italia imejihakikishia nafasi ya kwanza katika Kundi E na itakamilisha kazi ya kundi hilo kwa kupambana leo na Ireland ambayo lazima ishinde ili kuwa na nafasi yoyote ya kusonga mbele.

Nambari mbili Ubelgiji itacheza dhidi ya Sweden katika kile kitakuwa mchuano wa mwisho wa kimataifa kwa nyota wao Zlatan Ibrahimovic. Mshambuliaji huyo nyota mwenye umri wa miaka 34 atazitundika njumu za timu ya taifa ya Sweden la sivyo ishinde na kuoata nafasi ya tatu na kubakia Ufaransa kwa angalau siku kadhaa.

Viongozi wa Kundi F Hungary pia watafuzu, ijapokuwa sio kileleni mwa kundi lake baada ya kupambana na Ureno leo. Nambari mbili Iceland itachuana na Austria ambayo lazima ishinde. Orodha ya timu za nafasi ya tatu itajulikana baadaye leo.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef