1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cuba inapata kiongozi mpya wa dola

Miraji Othman26 Februari 2008

Haya ni mapinduzi ya kijamaa na ya kidemokrasia ya watu wa chini, ya watu wa tabaka ya chini, ya chini.

https://p.dw.com/p/DDRU
Fidel Castro(kushoto) na ndugu yake, Raul, ambaye ni rais mpya wa CubaPicha: AP

"Na sisi tuko tayari kutoa maisha yetu kwa ajili ya mapinduzi hayo ya kijamaa. Wafanya kazi na wakulima, wanaume na wanawake wanaapa kuyatetea mapinduzi haya hadi tone la mwisho la damu yao."

Hayo ni maneno ya kiongozi wa Cuba, Fidel Castro, alipotwaa madaraka huko Havana mwanzoni mwa miaka ya sitini na kwa miaka hamsini tangu wakati huo kuwa kwenye usukani wa uongozi wa nchi hiyo ya kikoministi ilioko katika Bahari ya Karibian, sio mbali na mwambao wa Marekani.

Lakini jumapili iliopita, Bunge la Cuba, lilimchagua Raul Castro, mwenye umri wa miaka 76 na ndugu wa Fidel Castro, mwenye umri wa miaka 81, kuwa rais mpya wa nchi hiyo. Tangu katikati ya mwaka jana Raul Castro alikuwa kaimu wa ndugu yake aliyekuwa anauguwa hospitalini. Na kutoka kwenye kitanda cha hospitali, Fidel pia alipiga kura kutaka ndugu yake achukuwe nafasi yake.

Rais George Bush wa Marekani alisema hivi kuhusu mabadiliko hayo:

"Suali hasa liwe vipi jambo hili litakavokuwa na maana kwa watu wa Cuba. Wao ndio walioteseka chini ya Fidel Castro, wao ndio waliotiwa magerezani kutokana na imani zao, wao ndio walionyimwa haki yao ya kuishi katika jamii ilio huru. Kwa hivyo nakiangalia kipindi hiki kuwa cha mpito kwa watu wa Cuba."

Machado Ventura, mwenye umri wa miaka 77, alichaguliwa kuwa makamao wa Raul; naye ni mwenye siasa kali. Yeye alipigana bega kwa bega na Castro wote wawili katika vita vya chini kwa chini vilivouangusha udikteta wa Batista na kufanikwa mapinduzi ya Cuba. Hiyo ina maana kwamba pindi Raul ataumwa au kufariki dunia, basi Machado atakamata urais. Nafasi ya spika wa bunge ikashikiliwa kwa mara ya nne na Ricardo Alarcon, mwenye umri wa miaka 70. Katika hotuba yake Raul Castro alimmiminia pongezi na sifa ndugu yake, akisema kiongozi mkuu wa mapinduzi ya Cuba anaweza kubakia tu kuwa mtu mmoja:

"Fidel ni Fidel, tunajuwa hivyo sisi vilivyo. Hamna mtu anayeweza kuwa sawa na yeye. Fidel Castro yuko pamoja nasi, kama maisha alivokuwa pamona na sisi. Fahamu yake iliokuwa wazi, kipawa chake cha kuchambua mambo, namna anavoona mbali mambo, sasa zaidi kuliko ilivokuwa kabla…"

Raul Castro hajaficha kwamba bado atategemea msaada wa kaka yake aliye mgonjwa:

"Naliomba bunge hili kwamba ninapochukuwa maamuzi yenye athari za muda mrefu kwa mustakbali wa taifa letu, na hasa linapokuja suala la kuilinda nchi, siasa za kigeni na maendeleo ya kiuchumi, basi niruhusiwe niendelee kushauriana na kiongozi wa mapinduzi, nishauriane na rafiki yetu na mwenzetu Fidel Castro."

Matumaini yaliowekewa Carlos Lage, mwenye umri wa miaka 56, atakamata nafasi ya pili ya uongozi wa nchi yaliyayuka. Kikao cha bunge hilo hakikifunga enzi katika Cuba, lakini kiliimaliza hatua moja ya enzi hiyo . Mfalme, yaani Fidel Castro, sasa ana mavazi mepya, badala ya sare ya kijeshi, sasa anavaa nguo za kufanyia mazoezi ya spoti, anabaki kuwa katibu mkuu wa chama pekee tawala nchini humo, mtungaji wa siasa za nchi na nguzo ya mrithi wake. Hivyo, kama ilivokuwa kabla, madaraka ya juu kabisa nchini Cuba yako bado mikononi mwa Fidel Castro.

Hali hii haijawafurahisha watawala wa Washington, kwani Cuba inabakia kuwa kama mwiba katika koo ya siasa za kigeni za Marekani. Tangu kuingia madarakani wakoministi huko Havana miaka 50 iliopita, chini ya Fidel Castro, marais kadhaa wa Kimarekani wamejaribu kuupinduwa utawala huo na kufanya njama ya kutaka kumuuwa Fidel . Lakini bila ya mafanikio. Ilipotangazwa kwamba Fidel anajiuzulu urais, Rais George Bush akiwa ziarani Afrika, alisema:

"Haya mabadiliko ya uongozi yafaa yafuatiwe na uchaguzi huru na wa haki. Na mimi nakusudia kweli uwe huru na wa haki, na sio chaguzi hizi za udanganyifu ambazo ndugu hawa Castro ati wanasema wameziendesha kidimokrasia."

Lakini picha sio moja kwa moja ya giza. Kabla ya mabadiliko haya ya wiki iliopita, Raul Castro aliwahi kutoa mwito kwa wananchi kutaja udhaifu iliokuweko katika jamii na kuja na mapendekezo ya kuboresha mambo. Na tangu wakati huo majadilinao yamekuwa moto moto, watu wamekuwa na ujasiri wa kutoa maoni yao. Heinz Dieterich, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya elimu jamii na aliwahi kufany akazi kwa karibu na Raul Castro, anataraji kwamba kutakuweko mabadiliko jumla kutokana na uongozi huu mpya:

"Cuba ni kama nchi inayoogopa kuumwa na nyoka, ukiangalia yale yaliofuata baada ya Mikhail Gorbaschov katika Urussi alipofungua milango ya kisiasa na ya kiuchumi kwa wakati mmoja. Na kutokana na mtizamo wa Cuba ni kwamba Mikhail Gorbaschov alishindwa kuudhibiti mwenendo na mambo yote, hivyo mambo yote yakapinduka. Lakini mimi nafikiri Cuba itasema: Sisi ni nchi ndogo na dhaifu kuelekea Marekani, na ili tusishindwe kuidhibiti hali ya mambo, kwanza tushughulike kuleta uliberali wa kiuchumi, labda kuendeleza ujasiri wa mali miongoni mwa wafanya biashara wadogo wadogo katika uchumi, pamoja na mambo kama hayo. Juu ya suala la nchi hiyo kujifungua, kisiasa, mimi nafikiri itategemea juu ya msimamo wa rais ajayo wa Marekani."

Hata hivyo, Raul Castro anahitajika sio tu kuifungua nchi hiyo, kiuchumi, lakini zaidi kuifungua milango ya magereza ya nchi hiyo. Kuna wafungwa wa kisiasa zaidi ya 200 katika nchi hiyo, na mmoja wao, Pablo Alvarez, aliyefunguliwa karibuni na wenzake wachache, anasema:

"Cuba ni jahazi inayozama, kwa hivyo inatufanya tusipande jahazi hiyo. Ili hali ya mambo iboreke, lazima mambo mengi zaidi yafanyike. Ilivokuwa serekali ya Cuba haiwapi haki wananchi kujiamuliwa njia ya kufuata na mustakbali wao, basi hakutakuweko mabadiliko. Hatuamini kwamba mambo yatakuwa vingine chini ya Raul Castro. Kuna mambo yanayokosekana. Hatusemi kwamba mambo yote yapinduliwe kutoka leo hadi kesho. Tunafahamu kwamba hali ya mambo katika Cuba ni ngumu mno, watu wetu lazima wapitie mzozo wa kutisha, mzozo wa kiuchumi, wa kijamii na wa kisiasa."

Lakini bado wako wanaobaki kuwa vichwa ngumu huko Cuba, kama vile waziri wa mambo ya kigeni, Perez Roque. Alipoulizwa vipi itakavokuwa Cuba bila ya Fidel Castro. Alijibu:

"Tena mapinduzi zaidi na tena ujamaa zaidi katika Cuba."

Duniani kumebakia nchi tatu tu za kikoministi, Cuba, Korea Kaskazini na Uchina. Tabaka mpya ya wazito wa kiuchumi huko Peking ambao wanaifanya nchi yao kuwa dola la kuogopwa hivi sasa duniani, kunaifanya Cuba kuionea gere Uchina. Ndio maana Raul Castro alisema kuuiga mfano wa Uchina si vibaya.