1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cuba kuadhimisha sherehe ya mapinduzi bila ya Fidel Castro.

Mohammed Abdul-Rahman26 Julai 2007

Ni kwa mara ya kwanza katika hisoria tangu mapinduzi ya 1959 , ambapo kiongozi huyo hatotokeza kwenye sherehe hizo.

https://p.dw.com/p/CHAT
Fidel Castro akipumzika hospitali anakoendelea kutibiwa.
Fidel Castro akipumzika hospitali anakoendelea kutibiwa.Picha: AP

Kwa mujibu wa tangazo katika gazeti la serikali Granma, sherehe hizo Julai 26, zitaongozwa na nduguye Rais Castro, Raul ambaye ana kaimu nafasi ya kiongozi wa taifa, makamu wa rais wa taifa na baraza la mawaziri.

Raul Castro ambaye ni waziri wa ulinzi amekua akikaimu nafasi ya Kiongozi wa Cuba , Kaka yake Fidel Castro tangu kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 81 alipomkabidhi madaraka kwa muda Julai 31 mwaka jana kwa sababu ya hali yake mbaya ya afya, ambapo alifanyiwa upasuaji mara kadhaa tumboni. Lakini pamoja na hayo duru rasmi nchini humo na hata magazeti hujiepusha kumtaja Raul kuwa rais wa muda au Kaimu Rais.

Sherehe za siku aya mapinduzi ni Julai 26, kuadhimisha kushambuliwa kwa kambi za Moncada na Carlos Manuel de Cespedes 1953 na kikundi cha vijana waliokua na silaha walioongozwa na Fidel Castro ambamo alikuwemo pia nduguye Raul mwenye umri wa miaka 76 asasa.

Huo ulikua mwanzo wa uasi uliomalizika Januari 1 1959 siku ya ushindi wa mapinduzi ya Cuba. Mwaka jana sherehe hizo zilihutubiwa na Castro binafsi siku nne kabla ya kulazwa hospitali.

Katika risala ya kukabidhi madaraka kwa muda, Castro alikabidhi majukumu mengine kwa kikundi cha uongozi wa pamoja akiwemo Makamu wa rais Felipe Perez Roque na hata rais wa benki kuu ya Cuba Fransisco Soberon Valdes

Tangu wakati huo Kiongozi huyo wa Cuba amekua akionekana katika picha za magazeti na kwenye televisheni tu. Hata hivyo tangu tarehe 29 Machi, Castro amekua akiandika juu ya fikra zake kuhusu masuala ya kitaifa na kimataifa katika makala inayochapishwa na gazeti la serikali chini ya kichwa cha maneno tafakari kutoka kwa kamanda mkuu-Komandante Fidel kama anavyoitwa na wafuasi wake.

Katika makala yake ya karibuni iliochapishwa Jumanne, Rais Castro alikiri kwamba wanamichezo watatu wa kikuba na mwalimu mmoja waliokua wakishiriki katika michezo ya bara la Amerika mjini Rio de Janeiro Brazil, wamekimbia na akasema “ Wanariadha wa kukodiwa katika jamii ya wanyonyaji.”

Kwa mtazamo wake, mabondia hao walioikimbia timu ya Cuba mwishoni mwa juma lililopita, huenda wamekubali kupokea mamilioni ya dola kutoka kundi la wahalifu linalowanunua mabondi na kuwauza ulaya.

Kwa jumla sherehe za mapinduzi Julai 26 mwaka huu zitakua za kwanza katika historia ya Cuba ambapo Fidel castro hatoshiriki na hotuba yake iatasomwa na nduguye Raul.

Wachambuzi kwa upande mwengine wanasema zingatio sasa ni uchaguzi mkuu utakaoanza kufanyika Oktoba wakianza kuchaguliwa wajumbe wa halmashauri za miji na kuendelea hadi ule wa mikoa na bunge la taifa. Utaratibu huo utamalizika mwaka ujao kwa uchaguzi wa bunge la taifa la wajumbe 609 na Baraza la mawaziri na baraza la taifa vyombo vyote viwili Fidel Castro akiwa ndiye mwenyekiti.

Hadi wakati huo Fidel Castro anaendelea kugonga vichwa vya habari na kushika hatamu katika taifa hilo la kijamaa-Cuba.