1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dalili njema zaibuka kwenye mkutano wa Mazingira wa Durban

29 Novemba 2011

Wakati mazungumzo ya Jukwaa la Mataifa 194 juu ya Mabadiliko ya tabia nchi (UNFCC) yakiingia siku yake ya pili mjini Durban, kuna dalili ya hatua za kupunguza athari za gesi chafu kutoka sekta ya usafiri wa baharini.

https://p.dw.com/p/13IqY
Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini akizungumza katika ufunguzi wa mkutano.
Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini akizungumza katika ufunguzi wa mkutano.Picha: dapd

Kwa mujibu wa tangazo lilitolewa leo (29.11.2011) kwenye mkutano huo, kuna uwezekano wa sekta ya meli kulipia ada ya uzalishaji wa gesi chafu unaofanywa na meli za kibiashara. Mpango huo unatajwa kuwa pia utazinufaisha nchi masikini.

Mkurugenzi wa Shirika la Mazingira na Kimataifa (WWF) anayehusika na sera ya kimataifa ya mabadiliko ya tabia-nchi, Keya Chatterjee, amesema hayo ni makubaliano ya kimsingi "lakini undani wake yakiwemo masuala ya kiwango cha ada hiyo unahitaji kuafikiwa katika vikao vyengine vya majadiliano".

Sekta ya usafiri wa baharini inachangia kiasi ya 3% ya uzalishaji wa gesi chafu ulimwenguni. Lakini, kama ilivyo kwa sekta ya usafiri wa anga, hadi sasa haina mkakati maalum wa kupunguza uchafuzi huu wa mazingira, jambo ambalo linapiganiwa sana na wanaharakati wa mazingira.

Bango la mwaka huu la mkutano wa kimataifa wa mazingira mjini Durban, Afrika ya Kusini.
Bango la mwaka huu la mkutano wa kimataifa wa mazingira mjini Durban, Afrika ya Kusini.Picha: UN/DW

Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo na Baraza la Kimataifa la Meli (ICS), WWF na Oxfam imesema uzalishaji wa gesi chafu unaofanywa na meli za kibiashara utawekwa kwenye kigezo cha masoko kama nyenzo ya kuupunguza.

Sehemu ya mapatano yatakayopatikana kutokana na ada itakayolipwa na sekta ya meli itakwenda kwa Mfuko wa Ulinzi wa Mazingira (Green Climate Fund), ambao nao utatoa kiasi ya dola bilioni 100 kwa mwaka kwa nchi masikini zilizo kwenye hatari zaidi ya kuathirika na mabadiliko ya tabia nchi.

"Baraza la Kimataifa la Meli, ambalo linajumuisha zaidi ya asimilia 80 ya makampuni ya meli za kibiashara, linapendelea zaidi kulipia ada ya moja kwa moja, lakini Shirika la Ulinzi wa Mazingira la Umoja wa Mataifa, linapendelea njia nyengine." Amesema Chatterjee, ambaye ameyaelezea makubaliano haya kuwa ni ishara njema, huku akirejelea hoja ya wanamazingira kwamba kushindwa kufidia gharama za uchafuzi wa mazingira unaofanywa na matumizi ya mafuta ya visukuku katika sekta ya usafirishaji "lilikuwa kosa kubwa sana".

Katibu Mkuu wa ICS, Peter Hinchliffe, amesema kuwa kanuni za ulipaji wa ada zinapaswa kutengenezwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) likiwa na viwango vinavyowiana kwa meli zote za kibiashara, bali kwa utaratibu unaoheshimu misingi ya matamko ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na mazingira.

"Ikiwa serikali zitaamua kwamba sekta ya meli lazima ichangie kwenye Mfuko wa Ulinzi wa Mazingira wa Kimataifa, hapana shaka sekta yetu itaunga mkono jambo hilo, ilimradi tu mchanganuo wake ukubaliwe na IMO kwa minajili ya fidia ya kibiashara kwa mafuta yanayotumiwa na meli na sio fidia ya jumla-jamala ya uzalishaji wa gesi chafu." Amesema Hinchliffe.

Mataifa ya Mashariki mwa Afrika, ambayo yanazungukwa na Bahari ya Hindi, ni miongoni mwa masikini kabisa ulimwenguni na yanayoathiriwa moja kwa moja na mabadiliko ya tabia nchi yanayochochewa na sekta ya usafirishaji baharini.

Ikiwa makubaliano haya yatatekelezwa, matarajio ni kuwa sehemu ya dola bilioni 100 kwa mwaka, itaelekea kwenye mataifa hayo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFP/Reuters
Mhariri: Othman Miraji