1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DAMASCUS: Ban Ki Moon aitembelea Syria

24 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC7V

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa; Ban Ki Moon, yumo mjini Damascus nchini Syria kwa mazungumzo na rais nchi hiyo, Bashar al Assad. Mazungumzo hayo yatatuwama juu ya juhudi za amani nchini Lebanon na eneo zima la Mashariki ya Kati.

Mazungumzo hayo pia yanatarajiwa kugusia mpango wa kuunda mahakama maalumu ya kimataifa itakayowahoji washukiwa wa mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Lebanon, Rafik Hariri, na kuingizwa kwa silaha nchini Lebanon kutoka Syria kwa njia isiyo halali.

Syria imeshutumiwa kwa kuhusika na mauji ya Hariri, dai ambalo serikali ya Damascus imekuwa ikilipinga.

Katibu mkuu Ban Ki Moon ameandamana na mjumbe wa Mashariki ya Kati, Terje Roed-Larsen, na maafisa wengine wa ngazi za juu kwa ziara ya siku moja ambayo ni ya kwanza tangu alipochukua madaraka kama katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Sambamba na taarifa hiyo, watu wasiopungua 15 wameuwawa na wengine kadhaa kujerihiwa wakati lori lililokuwa likisafiri kwa kasi lilipoyagonga magari 18 kwenye barabara ya kutoka Damascus kwenda Baghdad nchini Irak.