1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DAMASCUS: Nouri al Malik apinga shutuma dhidi ya serikali yake

22 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBWq

Waziri mkuu wa Irak Nouri al Malik amepinga vikali shutuma za Marekani dhidi ya serikali yake na amesema kwamba hakuna mtu yeyote aliye na haki ya kuiwekea mipango serikali iliyochaguliwa.

Bwana al Malik ameyasema hayo mjini Damascus mara baada ya kukamilisha ziara yake ya siku tatu nchini Syria. Waziri mkuu wa Irak amesema kwamba shutuma dhidi ya serikali yake zimetolewa kutokana ziara yake nchini Syria. Rais George Bush wa Marekani na balozi wake nchini Irak wote wameeleza kutoridhishwa na serikali ya waziri mkuu wa Irak Nouri al Malik.

Balozi wa Marekani nchini Irak Ryan Crocker ameulaumu utawala wa bwana al Malik kwa kutofanya jitihada za kupambana na hali ya migawanyiko baina ya madhehebu ya dini na pia kutafuta suluhu ya kitaifa amesema Marekani imevunjwa moyo sana kutokana hayo. Wakati huohuo takriban watu 15 wamuewawa katika shambulio la bomu la kujitoa muhanga katika mji wa Baiji kilomita 200 kaskazini mwa Baghdad. Watu wengine kadhaa wamejeruhiwa katika shambulio hilo.

Duru za hospitali zimesema kwamba wengi kati ya watu waliojeruhiwa ni raia.