1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DAMASCUS: Nuri al Maliki afanya ziara rasmi nchini Syria

20 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBXI

Waziri mkuu wa Irak, Nuri al Maliki amefanya mazungumzo na viongozi wa Syria mjini Damascus hii leo. Mazungumzo hayo yamelenga kuishawishi Syria kuacha kuwasaidia wanamgambo nchini Irak.

Nuri al Maliki ni waziri mkuu wa kwanza wa Irak kuitembelea Syria tangu uvamizi wa Irak ulioongozwa na Marekani mnamo mwaka wa 2003. Vita hivyo vimesababisha wimbi kubwa la wakimbizi wa Irak nchini Syria.

Nuri al Maliki ambaye aliishi miaka mingi nchini Syria akiwa uhamishoni kama mwanachama wa upinzani dhidi ya Saddam Hussein, amekutana na waziri mkuu wa Syria, Naji al Otari na anatarajiwa kukutana na rais wa Syria, Bashar al Assad hapo kesho.

Ziara ya Nuri al Maliki nchini Syria inafanyika kufuatia ziara aliyoifanya nchini Iran mwanzoni mwa mwezi huu, nchi ambazo zimelaumiwa na Marekani kwa kuchochea machafuko nchini Irak.

Akiwa ameandamana na mawaziri wake wa mafuta, biashara, maji na maswala ya ndani, Nuri al Maliki atakutana na makamu wa rais wa Syria, Faruq al Shara na waziri wa kigeni, Walid Muallem.