1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DAR ES SALAAM : Waafrika washikamana na Mugabe

30 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCEK

Viogozi wa Kiafrika wamekuwa na mshikamano na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe hapo jana na kupuuza wito wa kuchukuliwa kwa hatua kali dhidi ya kiogozi huyo badala yake imetaka nchi hiyo iondolewe vikwazo.

Mugabe amekuwa akizidi kukabiliwa na kususiwa na mataifa ya magharibi katika kipindi cha wiki mbili zilizopita baada ya polisi wake kuwakamata viongozi wa upinzani na kuwapa kisago kikali wakiwa mahabusu jambo ambalo limezusha wito wa kuwataka majirani zake kuongeza shinikizo dhidi ya utawala wake.

Badala yake mkutano huo maalum wa viongozi wa Jumuiya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC umeyataka mataifa ya magharibi kuacha kuiwekea vikwazo Zimbabe na kuitaka Uingereza kuheshimu ahadi zake kugharamia mpango wa mageuzi ya ardhi katika koloni lake hilo la zamani.

Viongozi katika mkutano huo pia wamemkabidhi Rais Thabo Mbeki wa Afrika jukumu la kuzima mgogoro wa kisiasa unaozidi kukua nchini Zimbabwe kwa kumsuluhisha Mugabe na wapizani wake.

Mwenyeji wa mkutano wa siku mbili ambao ulikuwa wa faragha Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania amesema jumuiya hiyo ya kusini mwa Afrika imezitaka pande zinazohusika na mzozo wa Zimbabwe kuzipa nafasi juhudi hizo na kujiepusha kuchukuwa hatua za kuichochea hali hiyo.