1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DAVOS:Washiriki wakubali kufufua mazungumzo ya Doha

29 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCWu

Mkutano wa masuala ya Kiuchumi uliofanyika mjini Davos,nchini Uswisi umekamilika huku washiriki wakiwa na mtizamo mzuri.Washiriki hao wameafikiana kufufua mazungumzo ya Biashara ya Ulimwwengu ya Doha jambo ambalo lilikuwa muhimu kabisa katika mkutano huo wa siku tano.Kansela wa Ujerumani Angela Merkel vilevile Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair kwa pamoja wanasistiza umuhimu wa kupiga hatua katika mazungumzo ya Doha ili kulegeza masharti ya biashara.

Bi Merkel kama kiongozi wa kundi la mataifa nane yaliyostawi kiviwanda G8 alisistiza hilo pamoja na kufutia mataifa ya Afrika madeni kuwa moja ya malengo ya mkutano wa G8 utakaofanyika mwezi Juni mwaka ujao nchini Ujerumani.

Kwa upande mwingine Rais wa palestina Mahmoud Abbas na Waziri wa mashauri ya kigeni wa Israel Tzipi Livni wanatangaza kuwa nchi zao zinajitolea kutafuta suluhu ya mvutano kati yao.

Mkutano huo wa siku tano uliwahusisha zaidi ya viongozi alfu 2 kutoka mataifa 90 wakiwemo marais 24 ,viongozi wa kibiashara vilevile wa mashirika yasiyo ya kiserikali.

Nchi za Uchina na India zinasisitiza kuwa zitaimarisha juhudi zake za kusafisha mazingira.