1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Davutoglu: Raia wa Syria anahusika na shambulizi Ankara

18 Februari 2016

Waziri Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu amesema raia wa Syria mwenye mafungamano na wapiganaji wa Kikurdi nchini Syria, amehusika katika shambulizi la kujitoa mhanga mjini Ankara na kuwaua kiasi ya watu 28.

https://p.dw.com/p/1HxFQ
Picha: Reuters/G. Garanich

Akizungumza leo na waandishi wa habari kwa njia ya televisheni, Davutoglu amesema kundi la waasi wa Kikurdi wa Uturuki linalojulikana kama Chama cha Wafanyakazi-PKK, ambalo limepigwa marufuku limeshirikiana na mwanaume mmoja raia wa Syria kufanya shambulizi hilo lililokuwa linaulenga msafara wa magari ya kijeshi, ambapo watu wengine kadhaa wamejeruhi.

''Kulingana na taarifa tulizizozipata shambulizi hili limefanywa na PKK kwa kushirikiana na raia wa Syria anayeitwa Salih Necar mpiganaji wa kundi la wakurdi wa Syria-YPG ambaye alijipenyeza kuingia Uturuki,'' alisema Davutoglu.

Gari lililokuwa na mabomu liliripuka jioni ya jana kwenye mji mkuu wa Uturuki, Ankara karibu na mabasi yaliyokuwa yamewabeba wanajeshi, ambayo yalisimama katika eneo la taa za kuongoza magari barabarani, kwenye eneo ambalo liko karibu na bunge na makao makuu ya vikosi vyenye silaha.

Davutoglu amesema watu tisa wamekamatwa wakihusishwa na shambulizi hilo na kwamba nchi yake itajibu mashambulizi hayo dhidi ya kundi la waasi ambalo limehusika na mashambulizi ya Ankara. Amewaambia waandishi wa habari kwamba serikali ya Syria ambayo ameituhumu kwa kuwaunga mkono wapiganaji wa Kikurdi nchini humo, ndiyo inapaswa kulaumiwa. Hata hivyo kundi la PKK limekana kuhusika na shambulizi la kigaidi la Ankara.

Moto ukiwa baada ya basi kushambuliwa Ankara
Moto ukiwa baada ya basi kushambuliwa AnkaraPicha: Reuters/Ihlas News Agency

Wanajeshi saba wauawa leo kusini amshariki mwa Uturuki

Wakati huo huo, maafisa saba wa usalama wa Uturuki, wameuawa leo baada ya bomu kilipuka kusini mashariki mwa Uturuki. Duru za kiusalama zimeeleza kuwa bomu hilo lilishambulia gari la kijeshi kwenye barabara kuu inayouunganisha mji wa Diyarbakir, mji mkubwa wenye Wakurdi wengi na wilaya ya Lice.

Katika hatua nyingine Waziri mkuu huyo wa Uturuki amewataka washirika wake kuacha kuliunga mkono kundi la kikurdi la Syria. Uturuki inakichukulia chama cha Demokrasia cha Syria na tawi lake la kijeshi kama magaidi, kwa sababu lina mafungamano na kundi la PKK. Hata hivyo, kundi hilo limekuwa likipambana na kundi la Dola la Kiislamu.

Marekani ambayo imesema kundi la YPG sio kundi la kigaidi, imekuwa ikiwaunga mkono wapiganaji katika mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria. Kundi hilo pia linaungwa mkono na Urusi katika mashambulizi ya anga dhidi ya kundi hilo lenye itikadi kali. Kundi la PKK limekuwa kwenye mgogoro na serikali ya Uturuki kwa zaidi ya miaka 30.

Ama kwa upande mwingine, jeshi la Uturuki limesema ndege zake zimefanya mashambulizi ya kuvuka mpaka kwenye maeneo ya Wakurdi kaskazini mwa Iraq, saa chache baada ya shambulizi la Ankara na kuwashambulia kiasi ya waasi 70 wa PKK.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE,APE, DPAE
Mhariri: Gakuba Daniel