1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

de Maiziere ataka hatua madhubuti za usalama EU

Admin.WagnerD8 Novemba 2010

Panapohusika suala la ushirikiano dhidi ya vifurushi vya mabomu Ulaya, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Thomas de Maizière ana msimamo mmoja tu: sheria kali na sio kujali gharama zake

https://p.dw.com/p/Q1mr
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de MaizierePicha: AP

Sasa abiria wa ndege hawana tena uhakika ikiwa ndege waliyopanda siyo iliyopakia kifurushi cha mabomu, maana wataalamu wa kutengeneza mabomu wamegundua njia ya kusafirisha sehemu ya milipuko yao kupitia mizigo ya abiria. Takribani asilimia 60 ya mizigo husafirishwa kupitia ndege za abiria, na kwa kuwa kunatakiwa kuwepo hatua madhubuti za kutunza usalama viwanjani, basi anasema Waziri Thomas de Maiziere, abiria ana haki ya kuamini usalama wake.

Anasema kwamba, iwapo kila abiria ataupeleka mzigo wake ukasachiwa na kuhakikiwa, basi atakuwa na uhakika wa usalama wake.

Lakini bahati mbaya hivyo sivyo ilivyo. Si kila kifurushi katika kila kontena hupitiwa, kikakaguliwa na kuhakikishwa usalama wake. Na sasa de Maiziere hataki jambo hili liendelee kuwa hivi katika siku zijazo. Ulaya kuna sheria kwamba ikiwa mkaguzi hakuridhika na usalama wa mzigo wowote ule, basi anaweza kuamuru ushushwe na usasambuliwe kitu kimoja kimoja. Ni sheria hii ndiyo ambayo de Maiziere anataka sheria hii ipewe nguvu na itekelezwe kuanzia sasa.

Kuna nukta tano ambazo Ujerumani inaamini zikifuatwa na Umoja wa Ulaya, anasema de Maiziere, suala la kitisho cha vifurusi vya mabomu kitaweza kudhibitika. Kwa mfano, madhali inawezekana kufuatilia mkufu wa wapi kifurushi kilitokea, kikapitia hadi kikafika kinakokwenda, basi hatua za udhibiti zielekezwe huko.

Lakini uchukuwaji wa hatua kali kama hizi hauridhiwi na mawaziri wengine wa Umoja wa Ulaya, maana wanaona kuwa kunapandikiza khofu isiyo na maana miongoni mwa raia wa Bara hili, na hivyo kuwafanya magaidi kupata muradi wao wa kuwafanya watu kuishi kwenye hali ya wasiwasi.

Kwa hivyo, hata kama kuna ulazima wa kuchukuliwa hatua za dharura na za pamoja kukabiliana na hali ya sasa, bado uchukuwaji wa hatua hizo usiwe ule uliovuuka mpaka, na ambao utawatisha zaidi watu badala ya kuwafanya wawe na matumaini.

Lakini, kwa ujumla, Umoja wa Ulaya unakubaliana na de Maziere, na kama anavyosema Waziri wa Mambo ya Ndani ya Ubelgiji, Annemie Turtelboom, Ujerumani ina kila hoja inapotaka hatua za haraka zichukuliwe leo kabla ya kesho, maana usalama wa raia wa Bara hili hauwezi ´tena kusubiri ngoja ngoja.

Ujerumani inapigania kwamba suala hili lifanyiwe kazi na timu ya pamoja ya Umoja wa Ulaya na hadi ifikapo mwakani, ruhusa ya kuzitumia hatua anazozipendekeza iwe imeshatolewa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Andreas Reuter/ZPR

Mhariri: Josephat Charo