1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

De Maiziere atetea hatua za polisi dhidi ya wakimbizi Saxony

22 Februari 2016

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere, ametetea hatua zilizochukuliwa na polisi dhidi ya wakimbizi kwenye mji wa mashariki wa Clausnitz.

https://p.dw.com/p/1HziH
Picha: picture alliance/dpa/R. Jensen

Akizungumza wakati wa mahojiano na kituo cha televisheni cha Ujerumani, ARD, Waziri de Maiziere amesema hatua zilizochukuliwa na polisi kuwatoa kwa lazima wakimbizi kutoka kwenye basi katika jimbo la Saxony na kuwapeleka katika makaazi ya karibu, zilikuwa sahihi. Ameongeza kusema kuwa hawezi kukosoa operesheni hiyo iliyofanywa na polisi.

Mkanda wa video umewaonyesha maafisa kwenye mji wa Clausnitz wakiwalazamisha wakimbizi watoke nje ya basi akiwemo mvulana wa miaka 14, baada ya kundi la waandamanaji wanaopinga wahamiaji kujaribu kulizua basi hilo lisiwasili. Mji ulio karibu na mpaka wa Jamhuri ya Czech, ndiyo yaliko makaazi mapya ya wakimbizi.

Tukio hilo limelaaniwa vikali na wanasiasa pamoja na umma nchini Ujerumani, ingawa mkuu wa polisi wa jimbo hilo, Uwe Reissman, ametetea hatua hizo, akisema ilikuwa ''muhimu kabisa'' kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa wahamiaji.

Kibao kinachoonyesha mji wa Clausnitz, Ujerumani
Kibao kinachoonyesha mji wa Clausnitz, UjerumaniPicha: picture alliance/dpa/H. Schmidt

Wakati huo huo, kwenye kipindi hicho cha mahojiano na wanasiasa kinachoitwa ''Bericht aus Berlin,'' Waziri de Maiziere amesema amekosoa tabia za watu wanaopinga wahamiaji, akisema kuwa hazikubaliki kabisa, kwani watu wanaokwenda Ujerumani kutafuta hifadhi kutokana na mateso, hawawezi kukaribishwa kwa chuki na unyanyasaji. Amewataka maafisa kuelezea hali halisi ya matukio yanayohusiana na wahamiaji.

Ujerumani yakumbwa na matukio ya aina hiyo

Ujerumani imekumbwa na matukio kadhaa kama hayo katika miezi ya karibuni, wakati ambapo nchi hiyo inakabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi wanaovuka mipaka kuingia nchini humo. Siku ya Jumamosi, moto uliwashwa kwenye hoteli ya zamani katika mji wa Bautzen, ambayo iliandaliwa kwa ajili ya makaazi ya wakimbizi.

Ama kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere, amesema uamuzi wa Austria kukubali kupokea watu 80 tu wanaoomba hifadhi kwa siku, huku ikiwaachia maelfu wengine kwenda kwenye nchi nyingine, ni dalili zisizo sahihi na haukubaliki.

Hotel iliyokuwa itumike kama nyumba ya wakimbizi, Bautzen
Hotel iliyokuwa itumike kama nyumba ya wakimbizi, BautzenPicha: Getty Images/S. Gallup

Ujerumani ina wasiwasi kwamba wengi wa wahamiaji hao wanakwenda moja kwa moja nchini humo, ambako kuna wasiwasi wa kuongezeka zaidi, baada ya nchi hiyo kupokea zaidi ya maombi milioni moja ya watu wanaoomba hifadhi kwa mwaka uliopita, hivyo kutoa shinikizo kubwa dhidi ya sera ya kufungua milango ya Kansela Angela Merkel.

De Maiziere amesema hatua hiyo haitofanikiwa kama baadhi ya nchi zinadhani kwamba zinaweza kulitatua tatizo hilo kwa kuipa Ujerumani mzigo zaidi, akiishutumu Austria kwa kushindwa kuwakagua vizuri wakimbizi ambao inawaachia waondoke.

Licha ya kupingwa vikali na Umoja wa Ulaya, siku ya Ijumaa nchi ya Austria ilianzisha kikomo cha wahamiaji 80 wanaoingia nchini humo kwa siku, ambao wanaruhusiwa kuomba hifadhi, huku ikiwaruhusu wahamiaji 3,200 kwa siku kuvuka mpaka.

Mwandishi: AFPE, APE, DPAE
Mhariri: Yusuf Saumu