1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DEG yasaidia kuchangamsha maendeleo ya kiuchumi

P.Martin9 Februari 2007

Nchi nyingi zinazoendelea hufungua milango yake kukaribisha uwekezaji wa binafsi kwa azma ya kuhimiza maendeleo.

https://p.dw.com/p/CHKR

Na kampuni nyingi za Kijerumani zinahamia nchi za ngámbo ili kuweza kushindana kibiashara na kujipatia masoko mapya. Lakini uwekezaji katika nchi za ngámbo una hatari zake pia.

Jumuiya ya uwekezaji na maendeleo ya Ujerumani kwa ufupi-DEG tangu takriban miaka 45 inagharimia uwekezaji wa kampuni za binafsi katika nchi zinazoendelea na hata mataifa ambako uchumi unanyanyuka kwa kasi kubwa.Kwa mfano katika mwaka 2006,jumuiya ya DEG katika juhudi ya kuchangamsha sekta ya binafsi,iliidhinisha kiasi cha Euro milioni 930 kwa ajili ya miradi hiyo.Kiwango kikubwa kama hicho kimeweza kufikiwa kwa sababu ya ile hali nzuri ya kiuchumi iliyokuwepo duniani.Kwani mwaka jana,uchumi wa nchi zinazoendelea ulikuwa kwa asilimia 7 na uwekezaji wa kigeni katika nchi hizo uliongezeka kwa asilimia 10-ikiwa ni kama Dola bilioni 370. Maendeleo kama hayo,yamedhihirika pia katika biashara za jumuiya ya DEG ambayo hutia sana maanani nchi za Kiafrika na hasa kwa vile hali ya mambo inaendelea vizuri katika eneo hilo.

Kwa mfano nchini Kenya DEG imeisaidia kampuni ya Panda Flowers ambayo hukuza mawaridi na inaendelea vizuri.Kampuni hiyo huajiri watu elfu kadhaa na hivyo huwapa nafasi ya kupata pesa kwa ajili yao binafsi na familia zao.

Barani Afrika,katika mwaka 2006 DEG vile vile ilisimamia gharama za miradi mbali mbali nchini Mauretania,Tanzania,Cameroon na Zambia katika sekta za fedha,kilimo,viwanda vidogo au miundo mbinu.

Mwaka jana,eneo jipya la biashara lililoshughulikiwa sana na DEG ni bara la Asia. Sehemu kubwa ya Euro milioni 388 zilizotolewa, ilikwenda Indonesia,China,Pakistan na India.Polte ameeleza kwanini hata China ambako uchumi unanyanyuka kwa kasi kubwa,ni miongoni mwa nchi kumi kuu za biashara mpya,katika orodha ya DEG.

Lakini DEG huwekeza pia katika nchi zinazosemekana kuwa ni maeneo ya kubahatisha sana na yenye mapato madogo kama vile Afghanistan, Bangladesh na Cambodia.Katika kundi la nchi kama hizo,DEG binafsi hubeba mzigo wa zaidi ya asilimia hamsini.