1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Demokrasia nchini Uturuki mfano kwa nchi za Kiislamu

Admin.WagnerD1 Oktoba 2012

Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesifu ukuaji wa demokrasia nchini mwake, na kusema kuwa chama chake kinachotawala kilicho na misingi ya Uislamu, kimekuwa mfano wa kuingwa kwa nchi za Kiislamu.

https://p.dw.com/p/16I1O
Tayyip Erdogan
Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/dpa

Akihutubia maelfu ya wajumbe na viongozi wa mikoa wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho siku ya Jumapili, Erdogan alisema zama za mapinduzi ya kijeshi katika taifa hilo la watu milioni 75 zimekwisha.

Mkutano huo ulimchagua Racep Tayyip Erdogan kukiongoza chama cha Justice and Development, maarufu kama AK Party kuwa kiongozi wake kwa muhula mwingine wa miaka mitatu bila upinzani. Huu ndiyo ulikuwa mkutano wake wa mwisho kama waziri mkuu na kiongozi wa chama hicho kwa vile sheria za chama hicho zinamzuia mtu kugombea uongozi kwa zaidi ya mihula mitatu mfululizo.

Source News Feed: EMEA Picture Service ,Germany Picture Service Waziri Mkuu Tayyip Erdogan akisalimiwa na wafauasi wake wakati akiingia katika mkutano mkuu wa chama tawala nchini humo cha AK.
Waziri Mkuu Tayyip Erdogan akisalimiwa na wafauasi wake wakati akiingia katika mkutano mkuu wa chama tawala nchini humo cha AK.Picha: Reuters

Waziri mkuu huyo ambaye anatizamiwa kugombea urais mwaka 2014, alisema katika hotuba yake iliyokuwa inakatizwa na vifijo vya mara kwa mara, kuwa huduma ni muhimu kuliko vyeo. Matamshi hayo yalitafsiriwa na wachambuzi kama dalili za wazi kuwa anataka kuwa rais wa kwanza kuchaguliwa na umma chini ya marekebisho ya katiba ya mwaka 2007 yanayoweka mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja.

"Shabaha yetu ni kusherehekea miaka mia moja tukiwa nchi ya Jamhuri ifikapo mwaka 2023, na baada ya hapo tutajitahidi kuijenga Uturuki kuelekea Jubili ya miaka alfu moja," alisema Erdogan.

Aahidi kushughulikia suala la Wakurdi

Katika hotuba yake iliyodumu kwa karibu saa mbili na nusu, na ambayo ililenga kubainisha ajenda ya chama chake kwa kipindi cha miaka kumi ijayo, Erdogan aliahidi kuirekebisha katiba ya Uturuki na kuanzisha ukurasa mpya kuhusiana na jamii ya wakurdi milioni 15 wa Uturuki. Viongozi mbalimbali wakiwemo rais wa Misri Mohammad Mursi, rais wa Kyrgystan Almazbek Atambayev, rais wa jimbo huru la Wakurdi nchini Iraq, Masoud Barzani na kiongozi wa Hamas Khaled Mashaal walikuwa miongoni mwa wageni waalikwa.

Rais Mursi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika Mkutano huo alikisifu chama cha hicho tawala kama chanzo cha hamasa kwa kanda. "Nimekuja kuonyesha si tu mapenzi yangu, heshima na uvutiwaji kwa njia ya ufanisi iliyochukuliwa na Uturuki, lakini kufikisha pia salamu za raia wa Misri na uvutiwaji wao kwa mafanikio mliyoyapata."

Waziri mkuu Tayyip Erdogan na rais wa Misri Mohammed Mursi.
Waziri mkuu Tayyip Erdogan na rais wa Misri Mohammed Mursi.Picha: Reuters

Chini ya uongozi wa Erdogan, chama cha AK kimefanikiwa kushinda uchaguzi mara tatu mfululizo tangu mwaka 2002, na kuhitimisha historia ya serikali dhaifu za muungano ambazo zilikuwa zikipinduliwa mara kwa mara na wanajeshi. Pato la mtu moja moja nalo limeongezeka mara karibu mara tatu na Uturuki imerejesha ushawishi wake kama dola kubwa katika kanda ya mashariki ya kati, huku wsahirika wake wakiutizama mchanganyiko wa utulivu wa demokrasia na na utamaduni wa Kiislamu kama njia ya mfano kwa kanda hiyo inayobadilikabadilika.

Mwandishi: iddi Ismail Ssessanga/rtre, afpe
Mhariri: Saum Yusuf Ramadhan