1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Demokrat washindwa kufuta kura ya turufu ya Bush

Mwadzaya Thelma3 Mei 2007

Wanachama wa Demokratik katika bunge la marekani wameshindwa kufutilia mbali kura ya turufu iliyopigwa na Rais Bush hapo jana inayopinga hatua ya kutangazwa kwa ratiba ya kuondoa majeshi yake nchini Iraq.

https://p.dw.com/p/CHEw
Rais Bush katika Ikulu ya Whitehouse
Rais Bush katika Ikulu ya WhitehousePicha: AP

Baada ya mkutano katika Ikulu ya White House Rais George Bush wa Marekani na vigogo wa vyama vya Democratik na Republikan wamekubaliana kupata muafaka kuhusu suala la Iraq hususan ufadhili wa mpango wake na ratiba ya kuondoa majeshi yake nchini humo.Kikao hicho kilifanyika baada ya Rais Bush kupiga kura ya turufu inayolazimu kutangazwa kwa ratiba ya kuondoka majeshi ya Marekani nchini Iraq kuambatana na bajeti ya ufadhili.

Baada ya mkutano huo pande zote mbili ziliafikiana kuidhinisha mswada muafaka ifikapo mwishoni mwa mezi wa Mei.

Kwa mujibu wa Spika wa Bunge Bi Nancy Pelosi muda umewadia kushirikiana pamoja ili kumaliza vita nchini Iraq.

Kauli hiyo inatolewa baada ya miezi kadhaa ya mabishano makali katika Ikulu ya White House ambayo nusura yazushe purukushani na kulaumiana kuhusu ugaidi.

Wanachama wa Demokratik kwa upande wao wanaendelea kudai kwamba Rais Bush hana mpango maalum wa kupata mafanikio nchini Iraq jambo ambalo linawaweka wanajeshi wa Marekani katika hali mbaya.

Takriban wanajeshi alfu 3 wa Marekani wamepoteza maisha yao katika vita hivyo baada ya kushambuliwa na wanamgambo.

Hapo jana pande zote zilijaribu kulegeza misimamo yao ili kufikia muafaka.

Hata hivyo Rais Bush alikataa kuidhinisha chagizo la kuyaondoa majeshi ya Marekani nchini Iraq na Afghanistan ifikapo Oktoba Mosi.

Kiongozi wa chama cha Demokratik Bwana Steny Hoyer ana imani kuwa bunge litapigia kura bajeti ya Iraq katia kipindi cha majuma mawili yajayo na kueleza kuwa chama chake hakina nia ya kubana fedha kwa ajili ya majeshi ya marekani yaliyoko huko.Hayo yote yanatokea tangu Rais Bush kutangaza ushindi wa majeshi ya Iraq na washirika nchini Iraq katika vita ambavyo vimedumu kwa miaka mine.