1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Der Klassiker" - Bayern ina miadi na Dortmund

Admin.WagnerD3 Aprili 2015

Bayern Munich dhidi ya Borussia Dortmund umekuwa mpambano muhimu katika misimu ya karibuni lakini mwaka huu, Dortmund wamekwama katikati ya msimamo wa ligi wakati wakijiandaa kupambana na watani hao wa jadi

https://p.dw.com/p/1F2Vl
Fußball 1. Bundesliga 10. Spieltag Bayern München - Borussia Dortmund
Picha: picture-alliance/dpa/Revierfoto

Dortmund wamezoea kushindana kileleni mwa Bundesliga katika miaka ya karibuni lakini wakati watakapowaalika mabingwa Bayern leo, watafanya hivyo wakiwa katika hali isiyokuwa ya kuridhisha.

Wakati Bayern wakiwa na msimu wa kufana kufikia sasa kwa kushindwa tu mechi mbili kati ya 26, Dortmund, walimaliza nusu ya kwanza ya msimu wakiwa katika vita vya kuepuka kushushushwa daraja.

Lakini hawajashindwa katika mechi zao saba zilizopita na hivyo kupanda hadi nafasi ya kumi na wanaonekana kuilenga nafasi ya kufuzu katika dimba la Europa League msimu ujao. Bayaern hata hivyo watakosa huduma za Arjen Robben na David Alaba wakati pia Franck Ribery akiendeela kuuguza maumivu. Hata hivyo huenda nahodha Philipp Lahm akarejea kikosini kucheza dakika 90 kwa mara ya kwanza tangu alipoumia mwaka wa 2014.

Jürgen Klopp Bayer Leverkusen - Borussia Dortmund
Kocha wa BVB atataraji kupata uungwaji mkono kutoka kwa mashabiki wa nyumbaniPicha: picture-alliance/dpa/Revierfoto

Kabla ya Bayern kushuka dimbani na Dortmund, nambari mbili Wolfsburg watalenga kupunguza pengo kileleni mwa ligi ikiwa watashinda nyumbani dhidi ya Stuttgart.

Nambari tatu Borussia Moenchengladbach, baada ya kuwabwaga Bayern katika mchuano wa mwisho, watasafiri kupambana na Hoffenheim wanaotafuta nafasi ya Europa League. Bayer Leverkusen ambao wako katika nafasi ya nne watakabana koo na washika mkia SV Hamburg. Utakuwa mchuano wa kwanza chini ya ukufunzi wa mkufunzi wa michezo Peter Knaebel, aliyechukua usukani kutoka kwa Joe Zinnbauer aliyepigwa kalamu. Hanover watacheza ugenini dhidi ya Eintracht Frankfurt.

Mechi nyingine za Jumamosi Werder Bremen watakuwa nyumbani kupambana na Mainz 05 wakati Freiburg wakipimana nguvu na Cologne.

Kesho Jumapili, nambari tano Schalke watahitaji pointi moja ili kuimarisha matumaini yao ya kucheza katika Ligi ya Mabingwa msimu ujao lakini wako mbele ya wenyeji wao Augsburg ambao wako katika nafasi ya sita na pengo la pointi moja. Paderborn watafunga kazi wikendi hii kwa kucheza na Hertha Berlin.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri:Yusuf Saumu