1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dhaka. Kimbunga huenda kimesababisha vifo 1,000.

17 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CImH

Nchini Bangladesh , maafisa wanahofia kuwa kimbunga Sidr kinaweza kuwa kimesababisha zaidi ya vifo 1,000. Maafisa na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada wamesema kuwa maelfu ya watu hawajulikani waliko. Mkurugenzi wa shirika la umoja wa mataifa la UNICEF Louis Georges Arsenault amesema kuwa watu wengi wamekufa kutokana na majeraha.

Vifo vingi vimetokana na ajali kwa kuwa upepo ulikuwa mkali sana . Nyumba hazikuweza kuhimili kasi ya upepo huo.

Wafanyakazi wa uokozi bado hawajaweza kuwafikia watu katika maeneo ya vijijini, na simu pamoja na umeme umekatika. Maafisa wamesema kuwa kimbunga hicho ambacho kilishambulia usiku kikiwa na upepo unakwenda kwa kasi ya kilometa 250 kwa saa kiliharibu miji kadha ya pwani na kuwalazimisha watu wapatao milioni tatu kuondolewa katika maeneo hayo. Mamia ya maelfu ya watu walilala usiku katika maeneo maalum yaliyotengwa na serikali. Wakati huo huo juhudi za kimataifa za kutoa msaada zinaendelea kuisaidia nchi hiyo ambayo inakumbwa na maafa kila wakati. Wizara ya mambo ya kigeni ya Ujerumani imesema kuwa itatoa kiasi cha Euro 200,000 kwa ajili ya msaada wa dharura.