1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dikteta mpya wa Misri

25 Agosti 2013

Baada ya mapinduzi ya Julai 3, Jenerali al-Sisi anaelekea kujilimbilizia madaraka ambayo ni makubwa kuliko hata yale aliyokuwa nayo mtangulizi wake Hosni Mubarak. Waandamanaji wa Udugu wa Kiislamu hawamuwezi tena.

https://p.dw.com/p/19Vqs
Dikteta mpya wa Misri, Jenerali al-Sisi
Dikteta mpya wa Misri, Jenerali al-SisiPicha: picture-alliance/dpa

Zipo kila dalili kwamba Jenerali Abdel Fatah al-Sisi, kiongozi wa jeshi la Mirsi ambaye aliongoza mapinduzi dhidi ya rais wa nchi hiyo aliyechaguliwa kidemokrasia, Mohamed Morsi, anaelekea kwenye mkumbo wa watawala wa kiimla katika eneo la mashariki ya kati. Hayo yanadhihirika katika mienendo yake baada ya mapinduzi hayo, na katika namna vyombo vya habari vinavyoshindana kumpa sura ya mtu asiye wa kawaida.

Kabla ya kutoa muda wa mwisho kwa waandamanaji wanaomuunga mkono Mohammed Mursi, Jenerali Abdel Fatah al-Sisi alipata motisha isiyo ya kawaida kutoka kwa mmoja wa wafuasi wake sugu, naye ni Ghada Sherif, mwandishi wa kike wa gazeti la kibinafsi na la kiliberali Al-Masri al-Youm, ambaye alisema yuko tayari kuwa mtumwa wa ngono wa kamanda huyo wa jeshi.

Hiyo inaweza kutoa sura ya viongozi wa zamani madikteta wa kiarabu, kama Saddam Hussein wa Irak na Hafez al-Assad wa Syria, ambao waliweza kung'ang'ania madarakani, wakisaidiwa na vyombo vya habari vyenye kuimba sifa zao, na wasomi wanaoamua kufuata upepo kama bendera.

Yote yalianza ghafla

Bila shaka tunazungumzia eneo la Mashariki ya Kati, ambako zaidi ya miaka miwili baada ya kuibuka vuguvugu la mageuzi, bado jeshi na vyombo vya habari vya ndani vimekubuhu katika kuendekeza utawala wa kidikteta, ukianzia na marehemu Muamar Ghadafi, hadi familia ya al Saudi inayoitawala Saudi Arabia, na ukoo wa al-Nahian unaotawala katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Waandamanaji mjini Cairo
Waandamanaji mjini CairoPicha: Reuters

Sisi anaungwa mkono na waliberali pamoja na watu wasiotaka kuingizwa kwa masuala ya kidini katika siasa, na vile vile wakristu wa madhehebu ya Orthodox. Wote hao walipigwa kikumbo mara sita na watu wenye misimamo ya kidini ambao ni mahiri kwa kufanya kampeni, mnamo kipindi cha miaka miwili na nusu ambamo Misri ilionja demokrasia.

Kwa watu hao, vifaru, bunduki za rashasha na vyeo vya kijeshi, ndio njia pekee inayosalia kuelekea Ikulu. Na katika njia hiyo wameonyesha ukiukaji mkubwa wa sheria, haki za binadamu na maadili ya kidemokrasia.

Demokrasia yakabiliwa na kitisho

Katika juhudi za kuyahalalisha mapinduzi yao nje ya makundi yanayowaunga mkono, makamanda wa jeshi la Misri wanatumia vyombo vya habari na njia za kisasa za mawasiliano kama vile mtandao wa kijamii wa Facebook, kumuonyesha jenerali al-Sisi kama mkombozi na kipenzi cha watu.

Mohammed Badie, kiongozi wa udugu wa kiislamu aliyekamatwa
Mohammed Badie, kiongozi wa udugu wa kiislamu aliyekamatwaPicha: Reuters

Wakati mwingine juhudi hizo zinajumuisha hata kujinadi kwa uongo. Kwa mfano, gazeti linalomuunga mkono jenerali huyo pamoja na kurasa za Facebook za watu wanaomuunga mkono, hivi karibuni vilidai kuwa Marekani iliituma meli yake ya kivita kuingilia katika mzozo wa Misri, na kwamba jeneral al-Sisi alitishia kuiangamiza meli hiyo, na wamarekani wakafyata mkia na kuondoka.

Kujitapa huko kunaleta kumbukumbu za miaka 40 ya utawala wa Muamar Gaddafi nchini Libya. Hata mavazi yake al-Sisi, ya sare za kijeshi zilizosheheni tepe, na miwani myeusi ambavyo anavipendelea siku hizi, vinamfanya aonekane kama Kanali Gaddafi.

Dalili nyingine inayoonyesha anakoelekea jenerali al-Sisi ni namna magereza ya nchi hiyo yanavyofurika wapinzani, na ukandamizaji dhidi ya vyombo vya habari vinavyothubutu kumkosoa. Hata rais Mohamed Mursi aliyepinduliwa alifungwa mwezi mzima bila kujulikana aliko, kwa madai kuwa alikuwa na uhusiano wa kijasusi na kundi la kipalestina la Hamas.

Kibaya zaidi lakini, Al-Sisi aliivunja katiba iliyoungwa mkono na asilimia 64 ya raia kupitia njia ya demokrasia, na kurejesha makachero wa polisi ambao wanachukiwa na wananchi wa Misri. Wanawake na wazee wenye mavazi ya kidini wamesimamishwa njiani na kunyanyaswa kutokana na imani yao.

Vyombo vya habari vinavyomilikiwa na matajiri na wakristu wa kikoptiki ambao ni wakereketwa wa jenerali huyo vimejaa miito ya kuwafanyia kila aina ya ubaya waandamanaji wanaomtetea rais aliyepinduliwa, huku vikipigia debe uungaji mkono wa farao mpya, al-Sisi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/IPS

Mhariri: