1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dk. Charlotte Mannya Maxeke - Mama wa uhuru Afrika Kusini

2 Januari 2018

Ingawa wakati mwengine anaitwa "mama wa uhuru wa weusi Afrika Kusini," Charlotte Mannya Maxeke ameondolewa pakubwa katika historia, na michango yake muhimu ndiyo kwanza sasa inaanza tena kuripotiwa.

https://p.dw.com/p/2qEAo

Maisha: Alizaliwa Aprili 7 mwaka 1871 au 1874, na sio mwaka wa kuzaliwa tu bali hata mahali alipozaliwa pia ni jambo ambalo halibainiki wazi, ila rekodi zinaonesha kwamba ni Fort Beaufort Cape Mashariki au Ramokgopa katika wilaya ya Polokwane mkoa wa Limpopo. Alifariki dunia Oktoba 16 mwaka 1939, na historia ya maisha yake iliposomwa iliishia na maneno haya, "alikuwa rafiki wa kila mtu na hakuna mtu aliyekuwa adui wake."

Anajulikana kwa: Anajulikaa kwa mambo mengi, sauti yake ya kuimba, kazi yake kanisa na kupigania haki za wanawake, kipawa chake cha kuzungumza, lakini pia kama mwanamke wa kwanza kabisa wa Kiafrika kwenda chuo kikuu na kupata shahada.

Anaheshimika kwa:  Maxeke alikuwa miongoni mwa wanachama wa kwanza na waliojishughulisha sana na chama cha ANC, Maxeke alikuwa miongoni mwa wanachama wa kwanza wa kike na ni jambo ambalo historia haikulitambua. Naibu rais wa chama hicho Cyril Ramaphosa alipokuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa kumbukumbu ya Maxeke mwaka 2015 alisema, Maxeke alikuwa mzungumzaji mzuri kiasi ya kwamba mmojawapo wa marais wa kwanza wa ANC Reverend Mahabane, alijiunga na ANC baadae baada ya kumsikia akizungumza.

Hata kabla ya hilo kutokea katika miaka ya 1920, wakati ambapo ilikuwa nadra hata kwa wanawake wa kizungu kuitwa kushikilia jukumu hilo, aliitwa na wizara ya elimu Johannesburg kutoa ushahidi wa masuala fulani na hatimaye akaandikwa kama afisa wa masuala ya mahakama na hakimu katika mahakama eneo hilo.

Ni wakati alipokuwa akisoma katika chuo kikuu cha Wilberforce Ohio, Marekani, ndipo Charlotte Mannya aliyekuzwa katika misingi ya tamaduni ya Kikristo, alipoamua kuchukua mwenendo wa Kanisa la African Methodist lililokuwa likikisimamia chuo kikuu cha Wilberforce. Kanisa hilo lililokuwa la Wamarekani weusi lililkuwa linapigania usawa wa kirangi, jambo ambalo linaendelea mpaka wa leo. Charlotte aliwaandikia watu wake nyumbani Afrika Kusini, na mjomba wake aliyekuwa muumini wa kanisa hilo, akawaalika Afrika Kusini waanze kazi ya umishonari nchini humo mwaka 1896.

Katika mojawapo ya hotuba zake kama ilivyogunduliwa na Zubeida Jaffar, Maxeke alisema, ..."wacha niwaambie hivi nyinyi wasichana, ni uzuri wa moyo na tabia utakaodumu mpaka utakapokwenda kaburini. Urembo ni mzuri iwapo unaambatana na mambo mengine."

Kwa wanaume alisema, "Tunataka wanaume ambao ni wakombozi wa wasichana wa taifa lao, ambao wanaweza kutegemea uwepo wao, tunahitaji wanaume ambao watajinyenyekeza ili taifa liweze kuwainua wawe nyota wa Afrika kwa miaka ijayo. Haya ndiyo mambo ambayo Afrika inahitaji. Haya ndiyo mambo ambayo wanawake wa Afrika wanalia na kuomba yafanyike."

Kazi ya Charlotte Mannya Maxeke ilikuwa mwamko mkubwa mno kwa kutafuta haki za wanawake Afrika Kusini. Hadhi yake ya kuwa mwanamke wa pekee mwenye elimu Afrika Kusini, na heshima aliyotaka apewe na viongozi wa wakati huo wa Afrika na Ulaya, inamaanisha kwamba alikuwa kielelezo chema sio tu kwa wanawake bali hata viongozi wengi wanaume, waliotaka Waafrika Kusini wote waelimike na wajitegemee.

Mwandishi: Jacob Safari

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman