1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dola kubwa zaujongelea Ukanda wa Gaza

Charo Josephat/IPS5 Aprili 2009

Lengo ni kuzuia uingizwaji silaha kinyume cha sheria

https://p.dw.com/p/HQPN
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiandamana na,kutoka kushoto, katibu mkuu wa NATO Jaap de Hoop Scheffer rais wa Poland Lech Kaczynski na rais wa Marekani Barack ObamaPicha: AP

Nchi tisa wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO zimekubalina mwezi uliopita kutumia uwezo wa kijeshi, ujasusi na kidiplomasia kupambana na silaha haramu zinazoingizwa katika Ukanda wa Gaza. Wachambuzi kutoka Misri wanaiona hatua hiyo kama njia yenye hila ya nchi za kigeni kutaka kulidhibiti eneo hilo.

"Itifaki hii mpya haihusiani na kuzuia uingizwaji wa silaha kinyume cha sheria katika Ukanda wa Gaza," amesema Tarek Fahmi, profesa wa sayansi ya siasa katika chuo kikuu cha mjini Cairo Misri na ambaye pia ni kiongozi wa idara inayohusika na maswala ya Israel katika taasisi ya kitaifa ya masomo kuhusu Mashariki ya Kati mjini Cairo. Fahmi ameliambia shirika la habari la IPS kwamba nchi tisa za jumuiya ya NATO zinataka kudumisha udhibiti wa kigeni katika mipaka muhimu ya Ukanda wa Gaza na bandari zake.

Mnamo Machi 13 mwaka huu, mkutano mkubwa ulifanywa mjini London Uingereza uliolenga kuratibu juhudi za kuzuia silaha haramu kupitia nchi kavu na baharini kuingizwa Ukanda wa Gaza unaotawaliwa na kundi la upinzani la Hamas. Miongoni mwa walioshiriki kwenye mkutano huo ni wajumbe wa ngazi ya juu kutoka nchi tisa za jumuiya ya kujihami ya NATO, zikiwemo, Marekani, Uingereza, Canada, Denmark, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Italia na Norway.

Mkataba umesainiwa

Mwishoni mwa mkutano huo wa London, wajumbe walisaini mkataba kuundwe mkakati unaofaa wa ushirikiano wa kimataifa, kusaidia hatua zilizochukuliwa na mataifa ya eneo hilo, ili kuzuia na kukomesha uingizwaji bunduki, risasi na sehemu za silaha katika Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa taarifa ya mwisho ya mkutano huo, serikali zilizoshiriki zina matumaini ya kuyatimiza malengo haya kwa kutumia hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kudhibiti bahari, kupeana habari na shinikizo la kidiplomasia. Taarifa hiyo ilisema jumuiya ya kimataifa ina jukumu kusaidia juhudi za kuzuia uingizwaji wa silaha, ikitambua kwamba juhudi za aina hiyo zinaweza kujumulisha diplomasia, ujasusi na sheria.

Mkutano wa London unafuatia mkutano uliofanyika nchini Denmark mapema mwezi Februari mwaka huu. Wanadiplomasia walio karibu na mazungumzo hayo wanasema mkutano wa tatu kufuatilia mkutano wa London unatarajiwa kufanyika nchini Canada mwezi huu wa Aprili kukamilisha mkataba huo.

Misri yakataa kuhudhuria mkutano wa London

Ingawa Misri ilipokea mwaliko rasmi kuhudhuria mkutano huo wa London, ilisita kutuma mjumbe. Palestina pia haikuwakilishwa kwenye kikako hicho, iwe ni kutoka upande wa serikali ya mamlaka ya ndani ya Wapalestina inayoungwa mkono na Marekani inayotawala Ukingo wa Magharibi wa Mato Jordan au upande wa kundi la Hamas linalotawala Gaza.

'Mark Regev, msemaji wa waziri mkuu wa Israel aliyeondoka Madarakani, Ehud Olmert, ameyapongeza makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa London. Regev amenukuliwa akisema, "Kanuni hiyo iko wazi. Jumuiya ya kimataifa itachukua hatua kuzuia usafirishaji wa silaha."

Mark Regev Spoksman for israeli Prime Minister
Mark Regev (kushoto)Picha: DW/Samar Karam

Lakini wachambuzi nchini Misri wanasema makubaliano hayo ni juhudi ya kichini chini kuifanya kuwa swala la kimataifa hatua ya kuzingirwa kwa muda mrefu kwa Ukanda wa Gaza.

Tangu mapema mwaka 2006 wakati chama cha Hamas kiliposhinda uchaguzi kwa wingi wa kura, Israel na Misri zimekuwa zikiifunga mipaka yao na Ukanda wa Gaza na kuzuia abiria na bidhaa, licha ya kuendelea kuzorota kwa hali ya kibinadamu na kuongezeka kwa mahitaji msingi miongoni mwa wakaazi milioni 1.5 wa Ukanda wa Gaza. Hali ya kibinadamu imezidi kuwa mbaya kufuatia harakati ya jeshi la Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza iliyodumu majuma matatu, ambapo zaidi ya Wapalestina 1,400 waliuwawa na miundombinu mingi kuharibiwa.

Gamal Mazloum, mtaalam wa maswala ya kijeshi na ambaye ni jenerali mstaafu wa jeshi la Misri, ameliambia shirika la habari la IPS kwamba mikutano hii ya kupambana na uingizwaji silaha kinyume cha sheria katika Ukanda wa Gaza ni mkakati mpya wa kuulenga upinzani wa Wapalestina. Mazloum amesema huku Marekani ikiiipa Israel silaha na msaada wa kijeshi bure, inataka kuwanyima kabisa Wapalestina nafasi ya kupata silaha za aina yoyote kuweza kujinda wenyewe.

Mikutano ya Denmark na London inafanyika baada ya mkataba wa amani kusainiwa katikati ya mwezi Januari mwaka huu, siku chache tu kabla rais George W Bush wa Marekani kuondoka madarakani.