1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dola kuu 4 zinazoinukia kiuchumi

28 Agosti 2009

China,India,Russia na Brazil kuzipiku kiuchumi dola za G-7 ?

https://p.dw.com/p/JJxw

Ukuaji -uchumi,masoko mapya na dola zinazoinukia kiuchumi-ni matamshi 3 yenye tafsiri moja:Yanaeleza dola mpya za kiuchumi zilizoibuka mwanzoni mwa karne ya 21 zenye uwezo mnamo mwongo ujao kubadili wezani wa nguvu za kisiasa ulimwenguni.Usoni kabisa, zinachomoza dola 4 zinazojulikana kwa ufupi:BRIC-yaani, Brazil,Urusi,India na China.

Dola hizo 4 za BRIC hazina ukosefu wa kujiamini.Pale marais wa dola hizo 4 walipokutana kati ya Juni, mwaka huu huko Jekateringburg,mji huo wa Ural,uligeuzwa haraka na rais Medwedejew kuwa shina la "siasa za dunia".

Inapofanyika mikutano ya kilele ulimwenguni, dola hizo haziachi kualikwa.Na hii ni ishara wazi kwamba, bila ya dola hizi zinazoinukia kiuchumi, hakuna kinachoweza kufanyika.Si ajabu kwahivyo kuona klabu ya nchi hizo 4 inazalisha 15% ya pato zima la dunia,13% ya biashara ya dunia na kwa akiba yao ya dala bilioni 2.8 zinadhibiti 40% ya fedha za kigeni zilizozagaa ulimwenguni.

Mtaalamu mkuu wa uchumi wa Deutsche-Bank Nobert Walter anaamini nchi hizo zina uwezo wa kubadili wezani wa nguvu ya uchumi duniani.Anasema:

"Ni wazi kabisa.Mnamo miaka 5 hadi 7 ijayo, mkondo huu utazidi kupata nguvu kuliko kudhofika.Uzito wa nchi hizi utashawishi maamuzi tangu ya kibiashara hata ya uwekezaji . Marekani na nchi za ulaya, mnamo miaka 5 ijayo, zitashughulishwa na kazi ya kurekebisha uchumi wao .Kwani, katika nchi hizo, jambo la kwanza ni kujenga upya taasisi zao,kulipa madeni makubwa na hii itaimarisha zaidi ukuaji wa wastani wa uchumi wa dola hizo zinazoinukia kiuchumi."

Mkondo huu tayari sasa unaonekana katika masoko ya hisa.Kwani, baada ya mwaka wa msukosuko 2008,hisa zimeanza kupanda mjini Sao Paulo,Moscow,Mumbai na Shanghai.Zimepanda kwa alama ya hadi 50% na kupindukia masoko ya hisa ya dola kuu .Bingwa wa uchumi wa US-Ivestment bank Goldman, Benki ya raslimali ya Marekani-Jim O`'Neill zamani aliagua kuwa dola hizo 4 zinazounda BRIC ifikapo mwaka 2050 zitazipita dola kuu za kiviwanda za magharibi (G-7) kwa pato lao la uchumi.Sasa lakini, amerekebisha O`Neill, Anasema hii itatokea mnamo miaka 20 hivi ijayo.Mtaalamu wa utafiti wa kiuchumi wa kijerumani Walter, hapo ana shaka shakla kidogo:Anadai:

"Naamini, ni India na China tu, ndizo zenye sifa za kuibuka dola kuu na tayari wakati huu, zina nguvu za kukua kwa uchumi wao.Dola hizo mbili, bila ya shaka yoyote, uchumi wao utaendelea kukuwa kwa kima cha 7% mnamo miaka 5 ijayo na hivyo kuwa gurudumu la kusukuma mbele uchumi wa dunia."