1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dola kuu 5 za Baraza la Usalama na Ujerumani

2 Septemba 2009

Zazingatia hatua gani kuichukulia Iran ?

https://p.dw.com/p/JNuO
Saed Jalili-mjumbe wa Iran-nuklia.Picha: AP

Wanachama 5 wa kudumu wa Baraza la Usalama la UM wakijumuika na Ujerumani, wamekutana leo huko Wiesbaden ,karibu na Frankfurt kuzungumzia mradi wa kinuklia wa Iran.Madhumuni hasa ya kikao chao, ilikuwa kushauriana tu juu ya hatua gani kuichukulia Iran-hii ni kwa muujibu wa msemaji wa wizara ya nje ya Ujerumani.

Iran jana ilitoa ishara kuwa itayari kujiunga na duru mpya ya mazungumzo kuhusiana na mradi wake wa kinuklia.Hii inafuatia kutolewa vitisho vya kuiwekea vikwazo zaidi kutoka dola hizo 5 pamoja na Ujerumani.

Mjumbe mkuu wa Iran katika mazungumzo juu ya mradi wake wa kinuklia, Saeid Jalili amesema kuwa,mapendekezo ya Iran yanayohusiana na maswali ya kisiasa,kiuchumi na usalama,yamerekebishwa upya na yako tayari kukabidhiwa kikundi hicho cha wanachama 5 wa Baraza la Usalama pamoja na Ujerumani.

Lakini,mashauri ya Iran yadhihirika hayatii maanani dai kuu la kundi hilo la dola kuu kwamba, iachane kabisa na mpango wake wa kurutubisha madini ya uranium.

Mkutano wa leo umeingiza wakuu wa hadhi ya juu kutoka wizara za nje za Urusi,China,Marekani,Uingereza,Ufaransa na wa nchi mwenyeji-Ujerumani.Wizara ya nje ya Ujerumani haikupokea taarifa rasmi ya Iran kwamba, itayari kuzungumza tena -hii ni kwa muujibu wa msemaji wake Jens Ploetner.

"Hadi Iran imefanya hivyo, hakuna badiliko juu ya msimamo usioridhisha wa Iran"-alisema.

Mapema wiki hii, Kanzela Angela Merkel na Rais Nicolas Sarkozy kwa pamoja waliitishia Iran kuwekewa vikwazo vikali zaidi ikiwa Teheran itashindwa kujiunga na mazungumzo kabla ya mwisho wa mwezi huu.Rais Ahmadinejad wa Iran,anatazamiwa kuhudhuria Kikao cha Baraza Kuu la UM baadae mwezi huu mjini NY na kuhutubia wajumbe.

Swali na mradi wake wa kinuklia ni mada pia ya mazungumzo katika shirika la nguvu za atomiki ulimwenguni huko Vienna,Austria.Katika mahojiano yaliochapishwa mapema wiki hii, mkurugenzi wake Mohammed El Baradei alisema fimbo ya vikwazo itumike tu kama silaha ya mwisho na isiwalenge raia wa Iran katika mzozano juu ya mradi wa kinuklia.

Matamshi hayo yanatofautiana na mahojiano yake na Idhaa ya BBC Juni, mwaka huu pale El Baradei,aliposema kuwa Iran inataka kuacha mlango wazi iwapo itataka baadae kuunda silaha ya kinuklia. Baadhi ya nchi zinahofia kuwa Iran inayoweka shughuli zake za kinuklia siri, inajiandaa kuunda bomu la nuklia ambalo mwishoe, laweza kutumiwa dhidi ya adui mkubwa -Israel.Iran binafsi imekuwa ikikanusha tuhuma hizo na inaendelea kudai kuwa mradi wake wa nuklia ni wa kiraia na ni wa amani.

Mwandishi: Ramadhan Ali

Mhariri: M.Abdul-Rahman