1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Donald Trump aapishwa rais wa 45 Marekani

Sekione Kitojo
21 Januari 2017

Donald Trump,ameapishwa rasmi kuwa rais wa 45 wa Marekani katika sherehe zilizofanyika jijini Washington na kuahidi kuwaunganisha Wamarekani wote pamoja na kuifanya nchi hiyo kuwa Dola lenye nguvu tena.

https://p.dw.com/p/2WAP4

Washington Amtseinführung Trump
Rais mpya wa Marekani Donald Trump akiwa pamoja na makamu wake wa rais Mike Pence (kushoto)Picha: Picture-Alliance/AP Photo/E. Vucci

Donald  John Trump aliingia  madarakani  akiwa  rais  wa  45  wa Marekani  jana  Ijumaa  na  kuahidi  kufikisha  mwisho  kile alichosema  kuwa  ni  umwagaji damu nchini  Marekani  wa  viwanda vinavyoota  kutu  na  uhalifu  katika  hotuba  yake  ya  kuapishwa ambayo  ni  tamko  la  siasa  kali  za  mrengo  wa kulia na  za kizalendo zaidi.

Akionesha  ishara  ya  ukaidi , Trump  amesema  wafanyakazi  wa Marekani wameathirika  mno  na  upelekaji  nafasi  za  kazi  nje  ya nchi.

Washington Amtseinführung Trump
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: Picture-Alliance/AP Photo/M. Balce Ceneta

"Kuanzia  siku  ya  leo na  kuendelea  itakuwa  Marekani  kwanza," rais  huyo  kutoka  chama  cha  Republican  aliwaambia  maelfu  ya watu  waliokusanyika katika uwanja  wa  taifa  kumshuhudia akichukua  madaraka  kutoka  kwa  Barack Obama  wa  chama  cha Democratic.

Pamoja  na  Obama  na  marais  wengine  wa  zamani watatu wakiwa  wameketi  karibu, Trump  aliushutumu  uongozi  wa  zamani wa  Marekani  wa  kuwatajirisha  maafisa  mjini  Washington  kwa mgongo  wa  familia  zenye  matatizo  nchini  Marekani.

Ukionekana  mgawanyiko  mkubwa  nchini  humo, maandamano dhidi  ya  Trump  yalifikia  hali  ya  purukushani  kubwa  mjini Washington. Wanaharakati  waliovalia  mavazi  meusi  walivunja madirisha  ya  vioo  ya  maduka , walizuwia  magari  kupita  na kupambana  na  polisi  wa  kuzuwia  ghasia  ambao  walijibu  kwa kurusha  mabomu  ya  kutoa  machozi na  mabomu  ya  kushitua. Polisi  walisema  zaidi  ya  cwatu 200  walikamatwa.

Washington Amtseinführung Trump Proteste
Wakati Trump akiapishwa maandamano yalikuwa yakiendelea mjini Washington waandamanaji wakipinga kuchaguliwa kwake.Picha: DW/V. Esipov

Watu wachache

Picha  zilizochukuliwa  kutoka  angani  za  kundi  la  watu wanaomuunga  mkono  Trump  katika  uwanja  wa  taifa zinaonesha kuwa  ni  watu  wachache  waliohudhuria  hafla  hiyo mchana  Ijumaa kuliko  ilivyokuwa  wakati  alipoapishwa  rais Barack Obama mwaka 2009.

Makadirio  ya  watu  waliohudhuria  hayakupatikana  mara  moja kutoka  kwa  polisi.

Hotuba  ya  baada  ya  kuapishwa  ilikuwa inaakisi  hisia  halisi  za Trump , ikiwa  mambo  mengi  aliyabeba  kutoka  katika  mikutano yake  ya  kampeni aliyofanya  mwaka  jana  akiwa  njiani  kuelekea ushindi  Novemba 8  dhidi  ya   mgombea  wa  chama  cha Democratic  Hillary  Clinton, ambaye  alihudhuria  sherehe  hizo  za kuapishwa  akiwa  na  mume  wake, rais  wa  zamani Bill Clinton.

Trump  alisema  Marekani  imevitajirisha  viwanda  vya  mataifa  ya kigeni  badala  ya  makampuni  ya Marekani, kugharamia  majeshi ya  nchi  nyingine  wakati  jeshi  la  Marekani  likiporomoka, na kutumia  mabilioni  ya  fedha  nchi  za  nje  wakati  miundo  mbinu  ya nchi  hiyo  ikiharibika.

Wasi wasi wa mataifa ya  kigeni

Wakati  Trump  akijinasibu  kama  bingwa  wa  Wamarekani wafanyakazi, kituo  cha  sera  za  kodi ambacho ni  kituo kinachotoa ushauri  bila  kujali  chama kinakadiria  kwamba  maendekezo  yake ya  kodi hayataongeza  deni  la kiasi  cha  dola  trilioni 7.2 la serikali ya  Marekani  katika kipindi  cha  miaka  10  ya  mwanzo , lakini mapendekezo  hayo  yanatarajiwa  kuwasaidia  tu  Wamarekani matajiri.

Washington Amtseinführung Trump Parade
Trump na mkewe na makamu wa rais Mike Pence(kulia) na mkewePicha: Picture-Alliance/AP/M. Heiman

Kuchaguliwa  kwake  kulipokelewa  kwa  wasi  wasi  na  wengi duniani  kote, kwa sehemu  kutokana  na  sera  za  kujitenga  za mambo  ya  kigeni. Katika  mahojiano  baada  ya   Trump  kuapishwa makamu  kansela  wa  Ujerumani Sigmar Gabriel  alisema, "kile tulichokisikia leo  ni  matamshi  mazito  ya  siasa  za  kizalendo."

Rais  wa  Mexico  Enrique Pena Nieto  alimpongeza  Trump  kwa kuampishwa, lakini  alitahadharisha  kwamba  utaifa, maslahi  ya kitaifa na ulinzi  wa Mexico  ni  masuala  ya  juu  kabisa.

Kiongozi  wa  kanisa  katoliki Papa  Francis  alimtaka  Trump kuongozwa  na mfumo wa  maadili, akisema  ni  lazima  kuwaangalia masikini  na  waliotengwa.