1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Donald Trump afanya uteuzi mpya

Isaac Gamba
22 Desemba 2016

Rais Mteule wa Marekani Donald Trump amemteua  bilionea Carl Icahn ambaye ni mmoja wa wakosoaji wa udhibiti uliopitiliza katika serikali ya Marekani kuwa mshauri maalumu katika mchakato wa marekebisho kadhaa ya sheria.

https://p.dw.com/p/2UiQ5
USA Donald Trump 'Thank You Tour'
Picha: picture-alliance/dpa/D. Anderson

Donald Trump amemteua pia Peter Navaro, ambaye pia ni mkosoaji mkubwa wa China, kuongoza baraza la taifa la biashara la ikulu ya White House, ambayo ni ofisi mpya itakayosimamia masuala ya biashara pamoja na sera za viwanda ikiwa ni moja ya mipango ya rais huyo mteule kufanya mageuzi katika sera ya uchumi ya Marekani.

Icahn mwenye umri wa miaka 80, ambaye pia ni mwanaharakati wa masuala ya uwekezaji, hatafanya kazi hiyo kama mwajiriwa wa serikali na hivyo hatopokea mshahara wala kubanwa na kanuni zinazohusiana na miiko juu ya watendaji wa serikali, ambazo pengine zingeathiri uwekezaji wake kutokana majukumu hayo mapya aliyokabidhiwa.

Trump amesema utawala wa Rais Barack Obama ulionekana kuwaminya wafanyabiashara wa Kimarekani na kusema ni wakati muafaka sasa wa kuondoa kanuni ambazo zinaonekana kuwabana wafanyabiashara na badala yake wapewe wigo mpana  wa kufanya kile wanachoweza kufanya, ikiwa ni pamoja na kutengeneza fursa za ajira na kuongeza tija katika usitawi wa jamii.

Bilionea Icahn anaripotiwa kuwa mmoja wa watu waliomsaidia Trump katika uteuzi wa nafasi ya wale watakaounda baraza lake la mawaziri.

"Carl alikuwa pamoja nami tangu mwanzo na kutokana na sifa yake ya kuwa  mmoja wa wafanyabiashara wakubwa duniani, hilo linazidi kunipa imani kubwa kwake," alisema Trump katika taarifa yake.

Uteuzi wa Narvarro kama kiongozi wa baraza linalohusika na usimamizi wa masuala ya kibiashara katika ikulu ya Marekani, unaashiria kuleta mageuzi katika uhusiano kati ya Marekani na China baada ya hivi karibuni kuzuka mvutano kati ya mataifa hayo mawili makubwa yenye nguvu za kiuchumi duniani.

Ni mwandishi wa kitabu kiitwacho " Kifo cha China "

USA Peter Navarro Professor Universität von Kalifornien
Peter Navarro Professa katika chuo kikuu cha CaliforniaPicha: Imago/Zumapress

Narvarro ambaye pia ni profesa katika chuo kikuu cha California ni mwandishi wa kitabu kiitwacho ''Kifo cha China" ambacho kinakosoa sera za China zinazolenga kunufaisha zaidi viwanda vyake kwa kuzuia uingizaji wa bidhaa kutoka Marekani.

Wakati wa kipindi cha kampeni, Trump aliahidi kuleta mageuzi katika sekta ya uzalishaji na kuongeza ajira katika sekta hiyo ambayo aanadai imekuwa ikinufaisha zaidi mataifa ya nje kuliko wamarekani huku pia akiponda kile anachodai  mfumo wa China  usio huru wa ushindani katika biashara.

Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya nje ya China imeonya kuwa mahusiano kati ya nchi hiyo na Marekani yanaonekana yatakuwa na changamoto mpya na njia moja wapo ya kuimarisha mahusiano hayo ni kila nchi kuheshimu masilahi ya mwenzake.

Ama kwa upande mwingine Kauli iliyotolewa na waziri wa mambo ya nje wa China, Wang Yi, inaashiria msimamo wa nchi hiyo  kuhusiana na suala linaloihusu Taiwan kuwa ni suala lisilojadilika kwa sasa ikiwa ni wiki kadhaa baada yaTrump kusema kuwa atalazimika kufanya tathimini upya  kuhusiana na sera za Marekani zinazohusu Taiwan.

Mwandishi: Isaac Gamba /AFPE/APE

Mhariri: Mohammed Khelef