1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dondoo muhimu za uchaguzi wa Ujerumani

Sylvia Mwehozi
22 Septemba 2017

Raia wa Ujerumani wanapiga kura siku ya Jumapili kulichagua bunge jipya Bundestag, Bunge hilo Jipya kisha litamchagua kansela katika miezi michache ijayo.

https://p.dw.com/p/2kXcX
TV-Duell Angela Merkel und Martin Schulz
Picha: picture alliance/Dpa/dpa

Chama cha Kansela wa Ujerumani Christian Democrats CDU kinaonekana kuchukua uongozi, kulingana na kura zote za maoni zilizofanywa. Lakini uchaguzi huu unaweza kubadilisha hali katika siasa za Ujerumani, kwa mara ya kwanza kabisa katika miongo kadhaa vyama sita huenda vikawakilishwa katika bunge jipya badala ya vyama vinne kama ilivyozoeleka kwahiyo itakuwa vigumu kuunda serikali imara. Na ni kwa mara ya kwanza pia tangu katiba ya Ujerumani kuundwa mwaka 1949,  chama cha siasa kali za mrengo wa kulia huenda kikaingia bungeni.  

Kama kura ya maoni ni kitu kitakachoaminika na kufuatiliwa chama cha Kansela wa Ujerumani Angela Merkel  CDU huenda kikashinda katika uchaguzi wa Jumapili. Kura ya maoni ya hivi karibuni inaonyesha chama hicho cha CDU kinaweza kujikusanyia asilimia 36 ya kura, lakini kura hizo hizo za maoni pia zinaonyesha kuwa wajerumani bado hawajaamua ni chama gani watakachokipigia kura. Hata hivyo Kansela Merkel alitumia mikutano ya kampeni zake za mwisho kuwaomba watu wajitokeze kwa wingi kupiga kura. "Tunaishi katika wakati wa shida, kwa hiyo hatuhitaji majaribio. Tunahitaji hakikisho na tunahitaji utulivu na udhabiti, lakini nguvu zetu zipo katikati, ndio maana kila kura itakuwa na uzito siku ya jumapili," alisema Merkel. 

Deutschland Plakate Bundestagswahlen 2017
Wagombea wa Ukansela Ujerumani Picha: Getty Images/S. Gallup

Kwa kawaida hakuna chama kinachoshinda wingi wa kura, na kuweza kuunda serikali peke yake. Kwahiyo chama cha Kansela Merkel CDU kinahitaji mshiriki katika muungano wa serikali hata kikiibuka cha kwanza katika uchaguzi huu. Katika miaka minne iliyopita Ujerumani iliongozwa kupitia serikali ya muungano kati ya CDU na chama cha Social Democrats SPD.

Aidha kura ya maoni inakiweka chama hicho cha SPD chini kwa asilimia 23. Kiongozi wa chama hicho Martin Schulz bado anasisitiza kuwa anataka kuwa kansela mpya wa Ujerumani. Martin Schulz anasema, "Angela Merkel anaimudu hali ya sasa ya Ujerumani, nchi tunamoishi kwa sasa, na tunafurahia kuishi ndani ya Ujerumani, yuko sahihi kabisa tunaishi vizuri na tunafurahia kuishi katika nchi hii. Lakini pia tunahitaji kuishi maisha mazuri ya kesho na ndio maana tunahitaji kuwambia watu ni mkondo gani tunaouchukua."

Huku hayo yakiarifiwa haijakuwa wazi kama chama cha Social Democrats kipo tayari kuendelea na muungano wa serikali na chama cha CDU iwapo kitaibuka kuwa cha pili katika uchaguzi huu. Kwa hivyo vyama vidogo huenda vikafanikiwa katika hili. Nchini Ujerumani chama kinaweza kutuma wawakilishi bungeni iwapo kitajipatia angalau asilimia 5 ya kura zilizopigwa. Katika bunge la sasa kuna vyama viwili vidogo, chama cha die Linke na kile cha kijani.

Deutschland Wahlkampf Martin Schulz, SPD in Köln
Martin Schulz mgombea wa SPDPicha: Reuters/W. Rattay

Bunge jipya hata hivyo huenda likawa na vyama sita. Kura ya maoni inaonyesha kwamba chama cha waliberali FDP  kina nafasi nzuri ya kuingia bungeni baada ya kuondolewa mwaka 2013. Na kwa mara ya kwanza tangu vita vya pili vya dunia chama cha siasa kali za mrengo wa kulia huenda kikaingia bungeni. Chama hicho ni chama mbadala kwa Ujerumani AFD kilichofanya kampeni ya kichochezi dhidi ya wahamiaji. Alexander Gauland ni mgombea kupitia chama hicho. "Watu wanaotoroka mapigano wana haki ya kuishi katika nchi hii kulingana na mkataba wa Geneva. Lakini hawapaswi kujumuishwa, wanapaswa kurejeshwa nyumbani baada ya mgogoro kumalizika. Lakini wengi wanaokuja hapa hawayatoroki mapigano wanataka tu kuwa na maisha mazuri," alisema Gauland.

Matokeo ya mwanzo ya uchaguzi yataanza kutolewa muda mfupi baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa saa kumi na mbili jioni saa za Ujerumani, huku matokeo ya mwisho yakitolewa usiku wa jumapili au mapema siku ya Jumatatu. Baadaye ndio kivumbi kikali kitaanza cha kuunda serikali dhabiti ya muungano iwapo vyama vya CDU na SPD havitaendelea na muungano wao. Hilo likifanyika bado kutakuwa na chaguo nyengine mbadala katika kutekeleza hilo.

CDU na FDP huenda wakaunda serikali iwapo wote watakuwa na kura za kutosha kuunda serikali. Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wanasema kwa mara ya kwanza vyama vitatu huenda vikaunda serikali ya muungano kwa mfano CDU, chama cha kijani na FDP.

Mwandishi: Amina Abubakar/Daniel Pelz

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman